The House of Favourite Newspapers

Mjukuu wa Nyerere: Sioni Sura ya Babu Yangu Kwenye Ile Sanamu

MJUKUU wa Baba wa Taifa, Mwl. J. K. Nyerere, Sophia Nyerere, amesema haoni sura ya babu yake kwenye sanamu iliyochongwa na kukabidhiwa kwa Rais John Magufuli hivi karibuni katika uzinduzi wa Hifadhi mpya ya Burigi, Chato.

 

Amesema hayo kwenye mahojiano na Kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds TV.

 

“Kiukweli sioni sura ya babu yangu kwenye ile sanamu, aliyechora anisamehe sina nia ya kumharibia biashara, babu ameshafariki hawezi kujizungumzia ila tuliobaki tunatakiwa tuwazungumzie, nilisema ni mapema sana Watanzania kumsahau Baba wa Taifa.

 

“Nikiwa mdogo nyumbani walikuja wazungu walimletea zawadi ya sanamu nakumbuka babu aliikataa, haikuwa moja tu zilikuwa nyingi, kuna siku ililetwa sanamu aliniambia naionaje nikamwambia huyu ni wewe ile sanamu ipo kule nyumbani Butiama, ” amesema.

 

Naye,Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema wana wataalam watakaoitazama sanamu hiyo na kujua kama ina upungufu na kurekebishwa.
“Kwa nia njema kabisa wizara yetu iliamua kumpa tuzo maalum Rais Magufuli ambayo ina maneno aliyoyasema Mwl. Nyerere mwaka 1961, lakini nimeona imezua mjadala sana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Hatuyapuuzi maneno na comment za Watanzania wenzetu ambayo yanahusiana na uumbaji wa lile sanamu, kama kuna mapungufu sisi ndio wenye dhamana ya kuangalia kama liko sahihi, Wataalamu tunao serikalini tutawaita watuelekeze kama kuna mapungufu yatarekebishwa.
“Vijana na wanasiasa wanaozungumza kwenye mitandao tunawashukuru kwa comment zao na tunawatoa wasiwasi kuwa tutalishughulikia, jambo ambalo limenifurahisha ni kwamba vijana bado wanaikumbuka taswira halisi ya Mwl. Nyerere, ni jambo kubwa sana kwetu kama taifa.
“Nimefurahishwa pia na mjadala wa faru Rajabu ambaye pia yupo kwenye mikono salama ya TANAPA na anaendelea kufanya kazi yake vizuri kabisa bila shida, tutatafuta mtoto wake mmoja machachari tutamleta kwenye Hifadhi ya Burigi Chato,” amesema.

Comments are closed.