The House of Favourite Newspapers

Mkata Umeme ameanza kuwa mtamu

zulu-mkata-umemeWaandishi Wetu, Gazeti la Championi Ijumaa, Desemba 30, 2016

Dar es Salaam

KIUNGO wa Yanga, Mzambia, Justine Zulu ‘Mkata Umeme’, taratibu ameanza kuingia kwenye mfumo wa kocha wa timu hiyo, George Lwandamina baada ya juzi Jumatano kuonyesha uwezo mzuri ndani ya dakika 30.

Zulu aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Zesco ya nyumbani kwao, juzi alicheza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu Bara tangu atue nchini mwezi uliopita.

Katika mchezo huo dhidi ya Ndanda ambao Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 4-0, Zulu aliingia dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Said Juma Makapu, na kusababisha shangwe kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru.

Championi Ijumaa lilimfuatilia ambapo kwa muda wote aliocheza, alipiga pasi 29, kati ya hizo, mbili ndizo zilizoharibika, huku akikaba na kuifanya Yanga kuimarika zaidi kwenye nafasi ya kiungo.

Mzambia huyo alifanya madhambi mara moja baada ya kumchezea vibaya Omary Mponda.

Baada ya mechi Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema: “Zulu tunazidi kumpa nafasi ili auelewe mfumo wetu na kuzoeana na wenzake, tunaamini siku si nyingi ataanza kucheza kwa dakika zote.

“Tunakwenda katika michuano ya Mapinduzi, mpaka tukirudi atakuwa tayari ameshaelewana na wenzake na kuwa msaada mkubwa kwa timu.”

Akiwa uwanjani hapo, Zulu alionekana akizunguka maeneo mengi ambapo alifanikiwa kukwapua mipira kadhaa na kuisambaza kwa wenzake.

Aidha, alionekana kuwa na maelewano mazuri na kiungo mwenzake Haruna Niyonzima kutokana na jinsi walivyokuwa wanapigiana pasi safi huku wakifuatana uwanjani hapo.

YANGA 4 – 0 NDANDA FULL TIME (MAGOLI YOTE)

Comments are closed.