The House of Favourite Newspapers

Mke amfanyia umafia mwanaye umafia

0

Mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Fauzia Abeid ‘Mama Timotheo’, mkazi wa Kimara-King’ong’o jijini Dar, anadaiwa kumfanyia umafia mwanaye, Timotheo ili kumkomoa mumewe.

Tukio hilo la kusikitisha lilijiri usiku wa kuamkia Jumanne iliyopita ambapo mama huyo aligombana na mumewe kwa njia ya simu na kuamua kufungasha kila kilichokuwa ndani kwake ikiwa ni pamoja na nguo za mtoto kisha kumuacha Timotheo akilia na kutimkia kusikojulikana.

Baada ya kunyetishiwa mkasa huo, waandishi wetu walitinga eneo la tukio wakianzia Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Kimara-King’ong’o ili kumuona mtoto huyo ambapo walikutana na jirani msamaria mwema aliyesaidia kulala na mtoto huyo hadi kukakucha.

MSIKIE JIRANI

Jirani huyo aliyejitambulisha kwa jina la Edwin Mandele alisema kuwa, ilikuwa majira ya usiku ambapo walisikia kilio cha mtoto lakini wakahisi huenda alikuwa na mama yake.

Alisema kuwa kilio hicho kilipozidi, walilazimika kwenda kuchungulia ndipo wakashangaa kumuona akilia peke yake chumbani.

“Katika kushangaa, alikuja mama mmoja (jina kapuni), akasema kuwa mama wa mtoto huyo ameondoka na kabla ya kuondoka alikwenda kumuomba amuachie mtoto kwa sababu hamtaki na anataka aondoke kabisa eneo hilo kitendo ambacho hakukubaliana nacho,” alisema jirani huyo na kuongeza:

“Mama huyo alituomba tumchukue mtoto tumsaidie, alale mpaka asubuhi kwa sababu yeye hakuwa na sehemu ya kumlaza.”

Mandele aliendelea kusimulia kwamba, yeye alikubaliana na mkewe, wakaenda kwa mjumbe wa mtaa huo, Peter Mwigelo kuripoti ambapo mjumbe aliwashauri ikifika asubuhi waende kwa mwenyekiti serikali ya mtaa.

Alieleza kuwa kulipokucha, serikali ya mtaa walimtafuta Fauzia ili afike kumchukua mwanaye lakini alikataa kwa madai kwamba hamtaki mtoto huyo.

“Baada ya kusema hamtaki mwanaye, tunafanya mawasiliano na baba yake ambaye yupo safarini Zanzibar kikazi,” alisema mwenyekiti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Demetrius Mapesi aliyempeleka mtoto huyo kwenye Kituo cha Polisi cha Mbezi-Kwayusuf ambapo mama huyo alifunguliwa jalada la kesi namba KMR/RB/12935/2015 -KUTELEKEZA MTOTO.

Leave A Reply