The House of Favourite Newspapers

Atimuliwa kisa mtoto mwenye magamba

0

Shani Ramadhani

WE mshukuru Mungu! Rose Joseph (19), mzaliwa wa Mkoa wa Mara anayeishi Kirumba jijini Mwanza amefukuzwa na mumewe akituhumiwa kuitia mkosi familia baada ya kuzaa mtoto Violeth (miezi nane) mwenye magamba (matatizo ya ngozi).

Mtoto Violeth akiwa na mama yake.

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Rose alisema, baba yake mzazi alimlazimisha kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 baada ya kuhitimu elimu ya darasa la saba, mwaka 2010.“Baada ya kuolewa nikaanza kunyanyaswa kwa kufanyishwa kazi ngumu kama kulima, kuchunga mifugo na nyingine nyingi. Baadaye nikapata ujauzito wa kwanza, nikalea ile mimba kwa tabu.

“Siku ya kujifungua nikapelekwa hospitali lakini sikujifungua, mume wangu akaamuru nirudishwe nyumbani ambapo nikawa napewa dawa za kienyeji kwa kuwekewa puani, mdomoni na sehemu za siri,” alisema Rose.Rose aliendelea kusimulia kuwa, baada ya kutumia dawa hizo hali yake ikawa mbaya, akarudishwa tena hospitali na kufanyiwa vipimo ambapo iligundulika mtoto alifia tumboni. Kwa kutumia mikasi, madaktari wakamtoa mtoto.

Rose hakuishia hapo, aliendelea kuliambia Uwazi kuwa, alipata ujauzito wa pili ambao aliteseka nao sana kwa kufanya kazi ngumu kiasi kwamba ilibidi arudi kwa baba yake ambaye naye alimfukuza.

“Nilirudi kwa mume wangu mpaka nilipojifungua. Nilishtuka sana kujifungua mtoto mwenye magamba mwilini. Niliporudi nyumbani nikakuta mume wangu ana mwanamke mwingine. Alivyoniona na huyu mtoto akaniambia nichague mawili. Niondoke kwake au mimi na mwanangu tuuawe.

“Ilibidi niondoke. Nikaanza kuombaomba pesa kwa wasamaria wema kwa ajili ya kumpeleka mtoto Hospitali ya Bugando kwa matibabu. Nilipofika, nilipata wakati mgumu kwa sababu sikuwa na mahali kwa kufikia.
“Ilikuwa nikipata mtu wa kunisaidia pa kulala, nakwenda naye lakini ikifika asubuhi huyo mtu akimwona mwanangu vizuri ananifukuza. Nikawa nahangaika mpaka nikaja kukutana na msamaria mwema mwingine ambaye hadi sasa naishi kwake na mwanangu.


“Hospitali wamenipa masharti ya namna ya kumtunza mwanangu kwamba nimpe chakula bora, mafuta yasiyo na harufu na kumbadilisha nguo mara kwa mara kwa siku.“Naomba Watanzania wanisaidie pesa nipange chumba na kupata mtaji wa biashara ndogondogo kwa ajili ya kuniwezesha kumtunza huyu mtoto,” alisema Rose kwa huzuni.
Naye Ibanda Manyonyi aliyejitolea kumhifadhi mama Violeth alisema yeye aliamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu Mungu amembariki kuwa na uzima japo hana uwezo wa kipesa.

“Kutokana na hali ya mwanaye ilivyo na alivyokuwa ananyanyasika na watu hapa mjini, mimi sikuona sababu ya kumuacha aendelee kuteseka na mtoto mdogo hivi ndiyo maana nikaamua niishi nao kama binadamu wenzangu,” alisema Manyonyi.

Kwa yeyote atakayeguswa na habari ya mama huyu awasiliane naye kwa namba 0757-665556.
Picha kwa hisani ya Nitetee Foundation kupitia kipindi cha Nitetee Sauti ya Mnyonge kinachorushwa Star TV.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply