The House of Favourite Newspapers

Mke atimuliwa msiba wa mumewe

1

IMG_1493Mke wa marehemu akilia kwa uchungu.

Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI
D AR ES SALAAM: Mjane aliyejitambulisha kwa jina la Salome Efraim (32), mkazi wa Mbagala Kuu jijini Dar anadai kutimuliwa na wifi zake katika msiba wa mume wake, Boniphace Mhingo (45) akidaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo hicho kilichotokea Januari 27, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wetu nyumbani kwake, Keko jijini Dar wiki iliyopita, Salome alisema yeye ni mke halali wa Mhingo kwani walifunga ndoa mwaka 2013 na walikuwa wakiishi pamoja Mbagala Kuu.

IMG_1500Jeneza lililobeba mwili wa marehemu likiandaliwa kwa ajili ya kuagwa.

Aliendelea kusema kwamba mumewe alikuwa akiugua tangu mwaka jana na yeye ndiye alikuwa akimuuguza huku akiwa mjamzito wa miezi tisa hadi ilipofika Oktoba, mwaka jana ambapo ndugu zake walimchukua na kwenda kumuuguzia kwao, Mbagala ambako alifikwa na mauti.

Salome ambaye alikuwa akizungumza huku muda mwingi akilia, alisema:
“Nilikuwa nimekaribia kujifungua ndiyo maana ndugu zake walimchukua. Muda wangu ulipofika nilikwenda Hospitali ya Mico Mbagala, Dar kujifungua lakini kwa bahati mbaya mtoto alifariki dunia.

“Sikuwa na nguvu ya kufanya kazi yoyote hali iliyonilazimu kwenda kupumzika nyumbani kwetu, Moshi (Kilimanjaro) kwani kipindi chote hicho hadi kujifungua hakuna aliyekuja kuniona upande wa mume wangu.

IMG_1497…..Mwi wa marehemu ukiagwa.

“Baada ya kupata nguvu, nilirudi Dar. Baadaye nilikwenda kumjulia hali mume wangu kwao lakini cha ajabu ndugu zake walinikataza nisiongee naye, eti mimi ndiye ninayemuua. Nilipatwa na hasira lakini sikuwa na la kufanya.

“Mume wangu pia alichukia kitendo cha mimi kukatazwa kuongea naye lakini hakuwa na nguvu ya kutoa amri. Niliondoka na kurudi kwangu Mbagala Kuu.

“Kabla mume wangu hajafariki dunia, alikuja shemeji yangu mmoja akaniambia nihame hapa nyumbani akidai wanataka kuipangisha hii nyumba ili wapate fedha za kumtibu mume wangu. Nilijisikia vibaya, ni ndugu wachache tu wa upande wa mume wangu ndiyo waliokuwa wananipenda.

IMG_1506“Siku hiyo niliamua kwenda kumjulia hali mume wangu na kumuuliza pa kwenda kuishi. Niliwasalimia ndugu waliokuwepo lakini hakuna aliyeniitikia. Wakanikataza kuongea na mpendwa wangu. Nikaenda kutoa taarifa kwa uongozi wa Kanisa Katoliki Mbagala Kuu, walishangazwa na kitendo hicho.

“Tukafuatana na baadhi yao na wasimamizi wa ndoa yetu hadi alipo mume wangu. Walipouliza, walijibiwa kuwa mimi nilimtelekeza ndugu yao. Basi tukaondoka maana hakukuwa na maelewano mazuri.

IMG_1509…..Wakiaga kwa simanzi.

“Mume wangu alipofariki dunia sikupewa taarifa na ndugu zake bali rafiki yangu mmoja. Nilikwenda msibani. Nilipofika walinikataza kulia, wakaniambia niondoke labda niende tena siku ya mazishi na hakuna kulia na sitatambulishwa kama mke wa marehemu.”

Ijumaa iliyopita, Salome alifuatana na ndugu zake kwenda kumzika mumewe (akiwa na waandishi wa habari hii). Walipofika, waliambiwa wakae mbali na waombolezaji wengine, wasubiri kuaga na kuondoka ambapo walifanya hivyo.

NDUGU WA MAREHEMU WANAJIBU
Baada ya kusikia maelezo hayo ya upande wa kwanza, waandishi wetu walimtafuta kaka wa marehemu aitwaye Andrew Cosmas ambapo alipoulizwa, alikiri kutokea kwa tukio la mwanamke huyo kutimuliwa kwenye msiba wa mumewe.

IMG-20160131-WA0000Marehemu Boniphace enzi za uhai wake.

“Ni kweli hilo suala lipo, ila subiri nitakupigia baadaye kukuelezea kwa kina,” alisema na kukata simu.

Hata hivyo, mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, Cosmas hakupiga simu kama alivyoahidi na hata alipopigiwa tena na mwandishi wetu, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

1 Comment
  1. Furaha mwasanga says

    hao wanataka kumzulumu mali walizochuma na mmewe, ndo maana walianza visa siku nyingi hawana lolote

Leave A Reply