The House of Favourite Newspapers

Mke hutulii halafu unataka mapenzi ya mume?

0

Asalaam aleykum wapendwa wasomaji wangu. Wiki iliyopita nilipata ujumbe kutoka kwa baadhi yenu wakinipongeza kwa mada yangu iliyotangulia, iliyowasema akinababa, kwa matendo yao yasiyofaa wanayofanya dhidi ya wake zao.
Leo nimeona ni jambo la msingi kuwageukie nyie akinamama wenzangu ambao kutwakucha mnatangatanga mitaani, mkiwa hamna muda kabisa wa kukaa na waume au familia zenu.

Mmoja wa wasomaji mwanaume amenieleza jinsi anavyotamani kupumzika na mkewe nyumbani, lakini mke hana muda, kila siku kwake ni mwendo, kama hayupo kazini, basi kwenye shughuli za kigodoro na kama si huko, atakuwa baa na marafiki.

Anadai kitu kibaya zaidi ni kuwa wana mtoto mmoja, sasa hata kama atahitaji kuongeza mtoto, wanahitaji nafasi, mke hana nafasi na mumewe amechoka, ameamua kulalamikia huku.

Sasa nikuulize wewe mwanamke kiguu na njia, ni kwa nini hukumaliza mambo yako kabla hujaingia kwenye ndoa? Unajikuta ukimnyanyasa mumeo kwa raha zako, hivi kwanza unawezaje ukamuacha mume amelala, wewe ukaenda baa kunywa, eti na marafiki?
Na yeye akiamua kwenda, hivi kutakuwa na ndoa hapo, sasa basi suala la ndoa tuliweke pembeni, je familia mtaweza kweli kuimudu, maana huenda ndiyo wale ambao wakiambiwa na majirani kuhusu vitendo vya watoto wao wana-shangaa kwa sababu muda wa kukaa na familia haupo.

Nikusihi mwanamke mwenzangu, hata kama utakuwa bize vipi usiache kuweka ratiba ya kuwa na mumeo pamoja na familia kwa jumla, ni  muhimu sana.

Mume ana nafasi yake na starehe na kazi vyote vina nafasi yake, usihusudu sana mitoko yako ukamdharau mume, kumbuka hata vitabu vya dini, vinakufundisha kumheshimu mume na ikibidi kuacha kila kitu kwa ajili ya kumfanya afurahi.
Sasa wewe unamnyanyasa utasema nini siku hiyo? Kumbuka mwanzo wa kuzurura sana ndiyo mwanzo wa usaliti, kwani mumeo kama hakupati ipasavyo na wewe humpati, unadhani itakuwaje sasa, hakuwezi kuwa na mapenzi ya dhati.
Kitakachoendelea ni ninyi kuzoeana kwa sababu mmeshakuwa wanandoa lakini yale mapenzi ya kuona huyu ni mume na huyu ni mke hayatakuwepo kabisa.

Leave A Reply