The House of Favourite Newspapers

MKE: NIMEBAKWA, NIMETOBOLEWA MACHO! – VIDEO

SHINYANGA unaweza kujiuliza ni unyama wa kiwango gani wa mtu kumbaka mwanamke, halafu kama dhambi hiyo haitoshi anamuachia na kilema cha maisha kwa kumtoboa macho.  

 

Bila shaka huu ni unyama wa kiwango cha kutisha na kusikitisha, lakini ndiyo aliotendewa mke wa mtu, Fatuma (jina jingine linahifadhiwa kwa ajili ya maadili) mwenye miaka 50, mkazi wa kijiji cha Nyambula Kata ya Ngogwa katika Halmashauri ya Mji Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.

 

Yawezekana tukio hilo unaweza kuliona ni la muda lakini alipoibuka mke huyo wakati wa kuadhimisha miaka 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia,iliyofanyika katika viwanja vya jeshi la polisi wilayani hapa na kusimulia kilichompata kila mtu aliyemsikiliza alijawa na simanzi. Karibu kusikiliza simulizi yake hii: “Tarehe 28/10/2014 wakati natoka kwenye shughuli zangu za kibiashara ndipo nilipokutana na baba mmoja, akanisalimia, ile naitika tu akanipiga mtama.

 

“Nilipoanguka akanikandamiza, nikajaribu kujitetea nguvu zikaniishia na kujikuta napoteza fahamu. “Basi akatumia mwanya huo kunibaka na mimi sikujua kilichoendelea kwa sababu sikuwa na fahamu. “Nilikuja kuzinduka siku ya pili nilipojaribu kutazama sikuwa naona kwa sababu yule mwanaume aliponibaka alinitoboa macho,” alisema Fatuma na kuwafanya wasikiliza ushuhuda wake kujawa na huzuni na kujiuliza mwanaume yule alikuwa na ushetani gani wa kumfanyia mke huyo wa mtu ukatili huo.

 

Fikiria; uko sehemu umebakwa na kutobolewa macho, huoni pa kwenda unafanya nini kujiokoa? Fatuma anasema alichokifanya: “Nikaanza kuhangaika bila kutambua wapi naelekea, walitokea wanafunzi wakanisaidia kunifikisha nyumbani kwa mume wangu.

“Baadaye nikachukuliwa kupelekwa hospitali ya Kolandoto kwa ajili ya kupatiwa matibabu, madaktari wakasema macho hayawezi kuona tena,” alisema Fatuma wakati akitoa ushuhuda wake mbele ya watu waliokusanyika viwanjani hapo. Wakati mwingine ni kweli dunia haina huruma; mtu kabakwa, katobolewa macho lakini mume ambaye ungetaraji angekuwa upande wake naye anatajwa kujitenga naye.

 

Anajitenga kwa staili gani? Msikilize Fatuma anasimulia alivyoachwa na mumewe: “Baada ya kuona nimekuwa mlemavu wa macho tena nikiwa na tukio baya la kubakwa mume wangu alinikimbia akaniachia watoto. “Mume wangu hakuenda mbali na hapa ninapoishi, akaenda kuoa mwanamke mwingine wakawa wanaishi naye huku mimi na watoto tukibaki tunahangaika.”

 

Aidha, Fatuma alilishukuru Jeshi la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na Ofisi ya Ustawi wa Jamii ambao wamekuwa wakimhudumia kutokana na yeye kupoteza uwezo wa kufanya biashara zake kama alivyokuwa akifanya zamani. Naye Ofisa Ustawi wa Jamii, Abrahamani Nuru alisema kuwa, Fatuma alikuwa na watoto 13, watatu walipoteza maisha, mmoja aliolewa na kuachika.

 

Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Annamringi Macha aliagiza jeshi la polisi kumkamata mume wa mama huyo na kumchukulia hatua zitakazomfanya alazimike kutunza watoto wake na siyo kumwachia mkewe kulea familia, huku akiwa hana uwezo.

 

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, licha ya kwamba mtuhumiwa wa ubakaji alijulikana na kufungwa jela miaka 17 kwa kosa la kubaka na kumtoboa macho mlalamikaji, anakusudia kuziomba mamlaka za juu zinazoshughulika na masuala ya kisheria kuangalia namna ya kuipitia upya kesi hiyo ili mtuhumiwa aendelee kukaa jela kwa kuwa kitendo alichokifanya ni cha kinyama na cha kusikitisha.

Comments are closed.