Mke Wa Askari Aliyemuua George Floyd Adai Talaka

Kellie Chauvin, mke wa Derek Chauvin askari anayeonekana kwenye video inayosambaa kwa kasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii, akiwa amemkandamiza shingoni kwa goti kijana George Floyd na kusababisha kifo chake kilichoibua vurugu kubwa huko Minnesota, Marekani, amedai talaka kutoka kwa mumewe huyo.
Mwanamke huyo ambaye pia anajihusisha kwenye masuala ya urembo na mitindo, akiwa amewahi kutwaa taji la Mrs Minnesota, amepeleka maombi ya talaka mahakamani, akieleza kwamba ameumizwa mno na ukatili uliofanywa na mumewe na kwamba hataki tena kuendelea kuishi naye.

Mwanamama huyo pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya George Floyd na watu wote walioguswa na ukatili huo na kueleza kwamba anaomboleza nao juu ya kifo cha mpendwa wao huyo.
Mambo yanazidi kuwa magumu kwa askari huyo, kwani licha ya kitendo chake hicho cha kikatili kulichosukumwa na ubaguzi wa rangi, kusababisha vurugu kubwa nchini Marekani hasa Minnesota, lakini pia amefutwa kazi na tayari amefunguliwa mashtaka ya mauaji ya bila kukusudia, sambamba na wenzake alioshirikiana nao kwenye tukio hilo.
Imeandikwa na Hashim Aziz kwa msaada wa mitandao.

