The House of Favourite Newspapers

MKE WA MBUNGE YAMFIKA MAZITO

IKIWA imepita takriban miezi 8 tangu aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani ‘Profesa Maji Marefu’ afariki dunia, mkewe mdogo aliyefahamika kwa jina la Alwiya Ahmed yamemkuta mazito, Gazeti la Ijumaa lina simulizi yake ya kusikitisha.  

 

Akizungumza na waandishi wetu katika mahojiano maalum yaliyofanyika ndani ya Ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar, Alwiya alisema tangu mumewe huyo afariki dunia, amejikuta akiteseka na wanaye alioachiwa huku akikosa msaada wa kueleweka kutoka kwa ndugu wa marehemu isipokuwa mtoto mkubwa wa Maji Marefu aitwaye Thomas Stephen.

 

MSIKIE HAPA CHINI;

“Mimi na Profesa (Maji Marefu) tulifunga ndoa ya Kiislam mwaka 2016 katika ofisi ya Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya yeye kubadili dini. Ndoa yetu ilitawaliwa na furaha kwa kipindi chote. Kila mmoja alifurahia uwepo wa mwenzake. “Tuliishi maisha yetu, mume wangu hakupenda sana kuniweka karibu na ndugu zake licha ya kwamba walikuwa wakijua kuwa nipo na mimi nilikuwa ni mke wa tatu halali wa ndugu yao. Tulijaliwa watoto wawili huku makazi yetu yakiwa ni Dodoma.”

MAMBO YABADILIKA

Mjane huyo aliendelea kueleza kuwa, baada ya kuishi maisha yasiyo na mushkeli kwa kipindi kirefu, mambo yalikuja kubadilika baada ya mumewe kufariki dunia, hali iliyomsababishia kuingia kwenye machungu yasiyomithilika.

 

“Mume wangu alivyofariki dunia ni kipindi ambacho nilikuwa nimetoka kujifungua. Ilibidi niende Korogwe kwa ajili ya taratibu za mazishi na mambo mengine yaliyohusu hatma ya maisha yangu na wanangu. “Nikiwa pale msibani nilianza kuona mazingira ya kutengwa, sikuwa nikishirikishwa kwenye baadhi ya vikao vilivyokuwa vikiendelea pale. Sikujali sana hasa ukichukulia kwamba nilikuwa mzazi. Hata hivyo, taa nyekundu ilishaanza kuniwakia kuwa, huko mbeleni mambo yatakuwa si mazuri.

 

”Basi nikavulimilia pale hadi 40 ikapita na hapo ndipo nilipoanza kuona mvutano kwenye suala la mirathi halafu sikuwa nikishirikishwa kwa namna yoyote wakati na mimi ni mke halali wa marehemu na nina watoto pia.

 

“Suala hilo la miradhi likaenda mahakamani, nikajua labda huko nitapata haki za wanangu, lakini suala hilo likawa limechukua muda mrefu huku kukiwa hakuna uwazi wa kinachoendelea. “Hata nilipojaribu kuongea na baadhi ya ndugu wa mume wangu, hawakuonekana kulitilia maanani suala la kutengwa kwangu, yaani kwa kifupi ilionekana kama vile sihusiki kwa namna yoyote ile.

HALI YAWA TETE

Akiendelea kusimulia maisha yake huku machozi yakimtoka, mwanamke huyo alisema alivyoona hivyo aliamua kurudi kwanza kwao, Mombasa nchini Kenya na huko ndiko alikoanza kuona giza kwenye maisha ya watoto wake kwani hakujua ni vipi angepata haki zao kupitia mali alizoacha mumewe.

 

“Kuanzia hapo hali ikawa ni ngumu, nikiwa Mombasa nikawa napata msaada mkubwa kutoka kwa Thomas (mtoto mkubwa wa marehemu). Kwa kweli amekuwa akijitoa sana, lakini mara nyingi huwa najiuliza, ataendelea kunisaidia hadi lini wakati na yeye ana familia yake?

 

“Lakini huwa najiuliza pia kwamba, ni kwa nini nilee wanangu kwa shida wakati enzi za uhai wa mume wangu aliwahi kusema mali zake zote ni kwa ajili ya wanaye? Pale Korogwe kuna ukumbi mkubwa unaitwa Mamba Club, kwa siku huwa inaingia shilingi 300,000 hasa siku za wikiendi, sasa jiulize tangu msiba umetokea, ni kiasi gani kimekusanywa, ni kwa nini wanangu hawapati chochote?

 

“Mimi tangu msiba utokee niliwahi kupewa shilingi 300,000 tu, naishi maisha magumu na sina kazi yoyote kusema nitaingiza pesa, unaweza kuona niko kwenye tatizo kubwa kiasi gani.”

 

NI NANI WASIMAMIZI WA MIRATHI?

“Ninachofahamu mimi baada ya ndugu kukaa, alichaguliwa yule mtoto mkubwa wa marehemu (Thomas) na mke mkubwa wa marehemu (Mama Grace) kuwa wasimamizi wa mirathi. Ikumbukwe marehemu alikuwa na wake watatu, mmoja alifariki dunia siku za nyuma tukabaki wawili. Kwa hiyo nilidhani katika mazingira ya kawaida na mimi ningekuwa kati ya wasimamizi, haikuwa hivyo. Nakasema niwe mpole nikiamini kwamba kwa kuwa suala litaenda mahakamani, wanangu watapata haki yao lakini hadi leo kimyaa. Kila unayemuuliza anakujibu visivyoeleweka.

 

“Pale Korogwe kuna kaka wa marehemu anaitwa Mzee Ngonyani, nilifikiri yule angekuwa msaada mkubwa kwangu lakini wapi, ni kama amekuwa upande mwingine, mimi nimebaki na Thomas ambaye saidia yake si kwamba anatoa kwenye mali za marehemu bali kwenye mfuko wake. Sidhani kama ni sawa,” alisema mke huyo wa marehemu.

KILIO CHAKE NI KWA JPM

Mjane huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, kwa hali ilivyo anaona anakosa haki za wanaye hivihivi hivyo kilio chake anakielekeza kwa Rais John Magufuli akiamini yeye anaweza kuwa msaada mkubwa kwake kuliko kwa mtu mwingine. “Hili suala la mirathi liko mahakamani kule Korogwe, lakini sioni mazingira ya haki kutendeka ndiyo maana nikaona nimuombe Rais Magufuli anisaidie.

 

Hawa watoto ni wadogo sana, mmoja ana miezi 8 na mwingine mwaka mmoja na miezi 8, bado wana safari ndefu, sasa endapo sitajua hatma ya maisha yao leo, watasumbuka sana baadaye na itakuwa ni aibu pia kwa watoto wa aliyekuwa kiongozi kuja kuishi maisha mabaya.

“Naomba tu Rais aingilie kati kwenye hili, ajue tu kwamba mambo hayako sawa baada ya kifo cha mbunge wake na mimi kama mke mdogo wa marehemu, nina hali mbaya,” anasema mama huyo.

 

MSIKIE KAKA WA MAREHEMU

Baada ya mke huyo wa marehemu kuanika dukuduku lake, Gazeti la Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta Mzee Ngonyani ambaye ni kaka wa marehemu ili kutoa ufafanuzi wa madai ya shemeji yake huyo. Alipopatikana alisema; “Kwanza sisi tunamtambua kama mke wa marehemu na suala la mirathi ndiyo kwanza tunalifuatilia ili kuona jinsi mali zinavyoweza kugawanywa kwa wake wote wawili.

 

“Kuhusu hilo la pesa ya ukumbi, tulishakaa na kukubaliana kwamba naye awe anapata mgao lakini ni kweli kwamba tangu kipindi hicho hakupata ila ndiyo tunaweka mahesabu sawa tuone nani achukue nini. Bahati mbaya mke mkubwa wa marehemu amepata msiba ila akirejea tutaweka mambo sawa.”

Endelea kufuatilia magazeti ya Global ujue muendelezo wa sakata hili. Pia mahojiano hayo unaweza kuyapata kupitia Global TV Online.

Comments are closed.