Mke wa mtu achanwa viwembe

dunia-katili

Akiwa na majereha baada ya kujeruhiwa kwa viwembe.

Gabriel Ng’osha
AMA kweli dunia katili! Mke wa mtu aliyejulikana kwa jina la Asha Idd (27), mkazi wa Tabata jijini Dar, amepata majeraha mwilini na kichwani kufuatia kuchanwa na viwembe na mtu aliyedaiwa kumkopesha fedha kiasi cha shilingi laki moja (100,000) na kushindwa kumrejeshea, Ijumaa Wikienda lina kisa na mkasa.

Duru za habari zilieleza kwamba, kabla ya kufanyiwa kitu mbaya hiyo, Asha alimkopesha rafiki yake aliyejulikana kwa jina la Jenny, shilingi laki moja lakini ilichukua muda mrefu katika kurudisha fedha hizo ambapo kila alipotakiwa kurejesha alisema hana.

dunia katili 2

Baada ya kupata matibabu.

Ilidaiwa kwamba, baada ya Asha kuona anazungushwa, siku moja aliamua kwenda nyumbani kwa mdeni wake huyo na kumuazima mashine ya kusagia matunda (brenda).
Kumbe ilikuwa janja yake, kwani alipopewa kifaa hicho, moyoni alisema amejilipa kutokana na usumbufu wa mdeni huyo.

Kwa upande wake, Jenny, habari zinasema, baada ya kuona siku zinakatika bila brenda yake kurudishwa, aliamua kuifuata lakini akaambiwa hawezi kupewa hadi arejeshe fedha anazodaiwa.

“Jenny aliondoka kimyakimya na kwenda dukani kununua viwembe kisha akampitia shoga yake aliyejulikana kwa jina moja la Vicky. Ndipo wakaenda kumvaa Asha kwa kumchanachana sehemu mbalimbali za mwili,” alisema mnyetishaji wetu.

Akiendelea kusimulia mkasa huo, mpashaji huyo alisema: “Asha aliumia sana, damu zilimtoka chapachapa. Akapelekwa Kituo cha Polisi Tabata (Dar) na kupewa PF-3 kisha kukimbizwa Hospitali ya Tabata ambako alipatiwa matibabu kwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa.”

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mume wa Asha aliyefahamika kwa jina la baba Rehema, alisema baada ya watu hao kufanya unyama huo walitoweka ndipo akapigiwa simu na wasamaria wema na kufika nyumbani kwake haraka.
“Nilipokea simu kuwa mke wangu amechanwa na viwembe, nikajitahidi kufika haraka nyumbani.

“Hata hivyo, bahati nzuri ninavyozungumza na wewe mwandishi, watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Tabata kisha kufunguliwa kesi ya kujeruhi yenye kumbukumbu namba TBT/RB/5679/2015. Waliwekwa mahabusu kwa siku kadhaa halafu wakaachiwa kwa dhamana,” alisema baba Rehema.
Ndugu, jamaa na marafiki wa Asha wanadai bado wanasubiri majibu ya daktari huku wakilishukuru jeshi la polisi kwa kazi waliyoifanya na kusisitiza kuendelea kumtendea haki ndugu yao ili iwe fundisho wa watu wengine wenye tabia kama hiyo.


Loading...

Toa comment