The House of Favourite Newspapers

Mke wa Mugabe Anayetisha Kwa Matanuzi!

0
Grace Mugabe (52) akiwa na mume wake.

JINA la Grace Mugabe (52), kwa sasa ni maarufu barani Afrika hadi nje ya bara hilo. Hii ni kwa sababu ametawala vyombo mbalimbali vya habari duniani kwa namna alivyomuingiza mumewe, aliyekuwa Rais Robert Gabriel Mugabe (93) wa Zimbabwe katika wakati mgumu kisiasa.

 

Amemfanya Mugabe akose amani na kuondoka madarakani bila kupenda. Sababu kubwa ni mkewe huyo kudaiwa ‘kumpeleka puta’ kiasi cha kumpangia mambo fulanifulani serikalini. Hili imeliudhi jeshi na viongozi wengine. Kwa kujikumbusha tu ni kwamba ndiye kiini hasa cha kusababisha jeshi lichukue nchi na kumweka chini ya ulinzi mkali Rais Mugabe na uzee wake huo.

Grace alimshinikiza mume wake amfute kazi makamu wa rais na bila kujiongeza, Rais Mugabe amkamtimua harakaharaka ili kumfurahisha mkewe. Aliyetimuliwa na Mugabe ni Emmerson Mnangagwa ambaye ni kipenzi kikubwa kwa wanajeshi, wanachama wa Chama cha ZANU-PF na viongozi wa serikali.

 

Ndiyo maana leo hii Zimbabwe imekuwa chungu kwa Mugabe, watoto na mkewe ambaye hadi sasa amefichwa mahali pasipojulikana nchini humo.

 

GRACE NI NANI?

 

Huyu ni mwanamke mrefu, mwenye umbo la wastani, lakini mtata. Alizaliwa Julai 23, 1965 nchini Afrika Kusini na alirejea Zimbabwe mwaka 1970 kuungana na mama yake, Idah Marufu. Grace ana elimu ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Kabla ya kuolewa na Mugabe, alikuwa ameolewa na Rubani Stanley Goreraza. Alizaa na Stanley mtoto anayejulikana kwa jina la Russell Goreraza. Mtoto huyo amezaliwa mwaka 1984.

 

WALIVYOKUTANA

Grace wakati huo akiwa msichana, alianza kufahamiana kwa ukaribu zaidi na Rais Mugabe wakati akifanya kazi kama sekretari katika ofisi yake. Penzi la Grace lilimnogea Mugabe na kushindwa kujizuia, hivyo ilipofika mwaka 1996, rais huyo aliamua kufunga naye ndoa. Ikumbukwe kwamba kabla Rais Mugabe hajamuoa Grace, alikuwa na mke wake, Sally Hayfro ambaye ametangulia mbele ya haki.

 

NDOA

Wakati wa ndoa yao, Rais Mugabe alifanya bonge la sherehe ambapo dola za Marekani laki sita (600,000) ziliteketea, huku Wazimbabwe wakiishi kwa shida. Kuanzia wakati huo, Grace Mugabe alikuwa ameonja utamu wa keki ya ikulu hivyo akawa haambiliki tena akijidai kuwa kila kitu kipo chini yake.
Hivyo alibadili kabisa mfumo wake wa maisha na kuanza kuishi maisha ya anasa na kufanya matanuzi ya kila aina kadiri alivyoona inampendeza.

 

MATANUZI

Grace mwenye watoto watatu na Mugabe, alianza kuponda mali kwa mwendo wa mruko akiwa hajui tena shida, kwa kujinunulia vitu vya gharama kubwa.

Mwaka 2002 alikwenda nchini Ufaransa, akiwa kwenye duka moja alijinunua vitu mbalimbali vikiwa na thamani ya dola za Marekani 120,000. Grace anasifika kwa kufanya matumizi ya bei mbaya. Wakati mmoja alitumia dola milioni 3 kwa ajili tu ya kumwandalia mwanaye harusi.

Grace Mugabe; Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni tu kabla mambo hayajamwendea mrama, alinunua gari aina ya Rolls-Royce kwa dola laki tatu (300,000). Lakini mwaka 2014 ndiyo alivunja rekodi kwa kununua vitu vya anasa vilivyogharimu dola za Marekani milioni

 

2. NYUMBA Ukiondoa matanuzi hayo, Grace anamiliki mali lukuki, zikiwemo nyumba za kifahari ambazo zimelalamikiwa mno, lakini serikali ya Mugabe iliziba masikio. Wakati kelele hizo zikiendelea, yeye hakuona aibu na badala yake alijitokeza kujibu mapigo kwa kusema “nimenunua kwa fedha zangu”. Ilidaiwa kuwa nyumba hizo zimejengwa kwa kutumia fedha za chama tawala (ZANU-PF) kama ‘asante’ kwa mke wa rais.

 

Anamiliki pia maeneo makubwa ya ardhi. Mali nyingine zipo Malaysia na mapema mwaka 2008 iliripotiwa kuwa alitaka kwenda kuishi huko pamoja na familia yake, lakini akabadili msimamo. Nyingine zipo Hong Kong ambako inaelezwa mtoto wao, Bona ndiko anakosoma. Mali hizi zilizua gumzo, lakini mjadala wake ulizimwa kimyakimya.

 

Grace Mugabe anadaiwa pia kujinufaisha na almasi zinazochimbwa katika machimbo ya Chiadzwa, Mashariki mwa Zimbabwe. Vyombo vya habari vilipojaribu kuhoji utajiri wake, vilitishiwa kushtakiwa ili vimlipe fidia kwa sababu ya kugusa mahali pasipotakiwa. WATOTO Haya ni machache kati ya mengi yanayomhusu Grace Mugabe mwenye watoto watatu na Mugabe ambao ni Chitunga, Robert Junior na Bona.

Makala: Julian Msacky, Dar

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply