Lucy Kibaki afariki dunia akitibiwa Uingereza
Lucy Muthoni Kibaki enzi za uhai wake.
NAIROBI, KENYA
LUCY KIBAKI aliyekuwa mke wa Mwai Kibaki ambaye alikuwa rais wa Kenya, amefariki huko London, Uingereza, alikokuwa akitibiwa.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta, mama huyo ambaye alikuwa hajisikii vizuri kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, amefariki katika Hospitali ya Bupa Cromwell ya London baada ya kupata matibabu ya awali nchini Kenya.
“Mama huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi hii hususani katika kuendeleza maadili ya uongozi na kuendeleza hali za wananchi wa kawaida nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kupambana na janga la VVU na Ukimwi, kazi ambayo aliifanya kwa juhudi na kuwatia moyo watu wengi,” ilisema taarifa hiyo.
“Kwa niaba ya Wakenya na serikali yangu, ninatoa rambirambi za kutoka moyoni na kumwombea ujasiri Mheshimiwa Mwai Kibaki, familia na marafiki zake,” iliendelea taarifa hiyo.
Lucy Kibaki akiongea na wanahabari baada ya kuandikwa gazetini.
Taarifa hiyo iliongeza kwamba mipango ya mazishi itatangazwa baadaye.
Marehemu ambaye jina lake kamili lilikuwa Lucy Muthoni Kibaki alizaliwa miaka ya 1940 huko Mukurwe nyakati za ukoloni na kuwa muumini wa Kanisa la Presbyterian Church of East Africa chini ya mchungaji John Kagai na Rose Nyachomba.
Alikuwa mwalimu kwenye Chuo cha Kamwenja Teachers College kabla ya kuhamia Kambui College. Alibadilisha kazi ya ualimu akiwa Kambui College ambayo kwa sasa inaitwa Kiambu Girls baada ya uhuru mwaka 1963 na kuanza harakati za kisiasa huku akimuunga mkono mmewe, Mwai Kibaki.
Lucy Kibaki ndiye First Lady wa kwanza Mkenya kuanzia 2002 hadi 2013 mmewe alipokuwa madarakani kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano.
Lucy na Mwai Kibaki wamejaliwa kuishi pamoja na kuzaa watoto wanne ambao ni Judy Wanjiku, Jimmy Kibaki, David Kagai, na Tony Githinji.
Lucy akiwa na Kibaki enzi za uhai wake.
Marehemu Lucy mbali na kuwa mtu maarufu wakati wa utawala wa mumewe, Mwai Kibaki, alijulikana pia kwa vituko vingi, ikiwa ni pamoja na pale alipomzabua kibao ofisa mmoja wa serikali katika Ofisi ya Rais aliyekuwa akitangaza katika hafla moja alipolikosea jina lake akilichanganya na jina la mwanamke mmoja aliyedaiwa kuwa mke wa pili wa Kibaki.
Tukio hilo lilitokea Desemba mwaka 2007 ambapo baada ya ofisa huyo kupewa ‘adhabu’ hiyo aliondolewa eneo hilo mara moja na maofisa wa usalama waliochukua picha za tukio hilo na kulifuta, ambapo Rais Kibaki aliendelea na hafla hiyo iliyokuwa ya utoaji zawadi bila kujali kilichokuwa kimetokea.
Vilevile, mwaka 2004 marehemu Lucy alianzisha patashika kubwa alipotoa taarifa kwa waandishi wa habari akipinga uvumi kwamba mumewe alikuwa na mke mwingine zaidi yake.
Isitoshe, mwaka 2005, alivamia chumba cha habari cha kituo kikubwa zaidi nchini humo akiwa na walinzi wake wenye silaha ambako alilalamika kwa kuandikwa vibaya magazetini.
Katika tukio hilo, alimtwanga mwandishi wa habari aliyejaribu kumpiga picha ambapo alichukua kwa nguvu simu, kamera, vitabu na karamu za waandishi wa habari katika vurumai hiyo iliyochukua muda wa ‘masaa matano’.
“MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU LUCY MAHALI PEMA PEPONI, AMEN”