The House of Favourite Newspapers

Mkemia Mkuu Aanika Mazito Kipimo cha DNA

mkemia-mkuu-wa-serikali

Stori: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY, GAZETI LA AMANI, TOLEO LA JANUARI 12, 2017

DAR ES SALAAM: Mkemia wa serikali (pichani) ameweka wazi mambo matatu ya kufanya kabla ya baba hajafika kwenye ofisi zake kupima kipimo cha kubaini uhusiano wa vinasaba vya uzazi (D.N.A), Amani linakujuza.

Akizungumza na Amani juzi, mkemia huyo msaidizi ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema mambo hayo ndiyo masharti huku yakionekana kuwa magumu kuliko masharti anayopewa mtu anayekwenda kupima virusi vya Ukimwi (VVU).

Kufuatia ndoa nyingi kuingia kwenye migogoro na hata kuvunjika na sababu kubwa ikiwa ni wanaume wengi kuwahisi wake zao kuchepuka na wanaume wa nje, Amani lilifunga safari mpaka Maabara ya Kupima D.N.A ya Hospitali ya Muhimbili (The Muhas Genetics Laboratory ) ili kujua idadi kubwa ya matokeo ya wanaokwenda kujiridhisha kwa kupima watoto wao.

dna-machine2 Mtambo wa kupimia DNA

Kwenye ofisi hiyo, Amani lilikutana na mmoja wa wakemia wa maabara hiyo ambaye alisikiliza shida yake.

Baada ya kuambiwa kuwa mwanahabari wetu alikuwa akitaka kujua takwimu ya watu wanaokwenda kujiridhisha na watoto wao kama ni asilimia kubwa ya majibu ikoje, mkemia huyo ambaye alikataa kutaja jina lake kwa kuwa yeye si msemaji rasmi wa jambo hilo alianza kuweka mambo hadharani.

“Ni kweli hiki ndicho kitengo maalum cha kupima D.N.A hapa Muhimbili lakini kwa sasa hatujaanza kuwapima wanaotaka kujua kama watoto walio nao ni wao au la. Hii D.N.A imegawanyika sehemu nyingi.

“Kwa kutumia D.N.A unaweza kubaini magonjwa kadhaa ikiwemo kansa na magonjwa mengine hayo ndiyo tunayodili nayo kwa sasa.

“Kupima damu ili kujua mtoto kama ni wako au si wako hilo tunaweza lakini hatujaanza, ingawa lina masharti makuu kama manne kabla ya kuwapima na kuwapa majibu.

dna-machine“Watu wakiona hilo bango hapo limeandikwa Laboratory Genetics wanakuja na watoto kutaka kupima. Mbaya zaidi unakuta baba mwingine anakuja na mtoto, ukimtazama tu unagundua kabisa kuwa ana

 mhemko na hasira. Unaweza kumpa majibu ambayo yanaweza kusababisha akamdhuru huyo mtoto.

“Unaweza kukuta hata huko alikomtoa amemuiba, yaani amemchukua bila kumjulisha mama yake wala mtu yeyote hivyo tunawarudisha na kuwaelekeza waende kwa mkemia mkuu.

“Hata hivyo, kiutaratibu kabla mtu hajapima D.N.A hasa kwa wababa wanaotaka kujiridhisha, lazima wazingatie mambo makuu manne.

“Kwanza awe na barua ya Serikali ya Mtaa anaoishi na kusudio la kufanya hivyo pasipo madhara. Awe na barua ya Ustawi wa Jamii ambayo inaonesha suala hilo limeshafika mezani kwao na wamejaribu kulishughulikia kibusara na kufikia hatua ya kufanya hivyo.

dna-moleculesMuundo wa DNA

“Awe na barua ya polisi ili tujiridhishe kuwa, suala hilo liko kiusalama na hakuna madhara yanayoweza kutokea baada ya majibu ya aina yoyote. Suala la mwishoni lazima mpimaji amuangalie huyo muhitaji majibu kama hana dalili za muhemko maana mtu mwingine anaweza kupata majibu mabaya na kuanzisha mambo mengine.

“Unaweza kukuta baba ameshatumia gharama kubwa kumlea mtoto kwa muda mrefu halafu akute amelea mtoto asiye wake, ukweli inauma. “Kwa hiyo ukishatimiza mambo hayo manne unakwenda kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kupeleka sampo kwa ajili ya kupima,” alisema mkemia huyo.

Baada ya mkemia huyo kuweka bayana mambo hayo, Amani lilikwenda Ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) zilizopo Ocean Road jijini Dar kwa ajili ya kuzungumza na mkemia, Profesa Samwel Manyale lakini mmoja wa wasaidizi wake alisema bosi wake ametoka kikazi.

“Mmepishana hapa sasa hivi, wakati mnaingia, yeye anatoka! Kwani mlikuwa na shida gani?”

Amani lilimweleza msaidizi huyo kama angeweza kutoa takwimu ya waliokwenda kupima D.N.A mwaka jana ili kubaini uhalali wa watoto wanaoishi na baba zao.

“Aaah… hilo ni vizuri ungekutana na mkemia mkuu mwenyewe ndiyo angekujibu vizuri. Hata hivyo, kwa suala hilo inabidi uandike barua, atakujibu kimaandishi,” alisema msaidizi huyo.

Comments are closed.