The House of Favourite Newspapers

Mkenya Anaswa Akitoa Hongo Apatiwe Cheti cha Corona TZ

0

RAIA wa Kenya, Alexander Mwikali (42), amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya Sh. 200,000 kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, ili ampatie cheti cha uthibitisho wa kutokuwa na ugonjwa wa Corona.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, amesema raia huyo anaishi Nkuhungu jijini Dodoma na anafanya kazi kama mtaalam wa nyama wa Kampuni ya Alkafil.

 

Kibwengo amesema raia huyo alinaswa baada ya kuandaliwa mtego ofisini kwa Mganga Mkuu huyo alipokuwa akitoa rushwa ya Sh. 200,000 kinyume na kifungu namba 15(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 ili apate cheti hicho.

 

“Mtuhumiwa huyo alifikishwa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma na kufunguliwa shtaka husika ambalo alikiri na kutozwa faini ya Sh.500,000 na fedha aliyotoa kama hongo ikitaifishwa,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, TAKUKURU inawashikilia wanafunzi 13 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Dodoma kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani wa marudio wa somo la Applied Statistics II kwa mwaka wa tatu uliofanyika Novemba mwaka jana.

 

Pia, taasisi hiyo imetaja sekta vinara kwa kuongoza kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ambapo serikali za mitaa inaongoza kwa asilimia 23 ikifuatiwa na mikopo-umiza kwa asilimia 20.

 

Kibwengo ametaja taasisi zingine kuwa ni sekta ya ardhi asilimia 14 huku vyama vya siasa au uchaguzi, polisi na afya zikilalamikiwa zote kila mmoja kwa asilimia sita.

 

Sambamba na hilo, taasisi hiyo imebaini kuwa baadhi ya kampuni za ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji hukwepa kodi ya ushuru wa huduma, hali inayozikosesha halmashauri mapato stahiki.

 

Leave A Reply