Mkitoka Mkatambike! Matajiri 6 Waunganisha Nguvu Yanga

IMEFICHUKA kuwa viongozi wa Yanga wameunda kamati mpya ya Mipango na Ushindi inayoongozwa na mabilionea, Rais wa Makampuni ya GSM, Gharib Said Mohammed na mfanyabiashara mkubwa na maarufu, Rostam Aziz.

 

Hiyo yote ni katika kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri ya ushindi wakati wakiwania taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Hii imekuja zikiwa zimebaki siku tano kabla ya kuwavaa watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Yanga imepania na imelenga kuhakikisha msimu huu inaupoka ubingwa wa ligi kutoka mikononi mwa Simba ambayo imeutwaa mara tatu mfululizo. Mkitoka mkatambike…

Timu hiyo ina mwendo mzuri hadi hivi sasa ikiwa imefanikiwa kucheza michezo nane huku ikifanikiwa kushinda saba na kutoa sare moja dhidi ya Tanzania Prisons.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kamati hiyo tayari imeanza kufanya kazi tangu mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Prisons.

 

Mtoa taarifa huyo aliwataja matajiri wengine waliomo kwenye kamati hiyo kuwa ni Seif Magari, Abdallah Bin Kleb, Rogers Gumbo na Davis Mosha wanaojua mipango.

 

Aliongeza kuwa kamati hiyo inahusika kwa ajili ya kuongezea morali wachezaji na benchi la ufundi, ikiwemo posho na inaelezwa kuwa posho sasa zinatoka kwa wakati na zikilenga wachezaji na benchi la ufundi.

“Kamati ya vichwa sita imeundwa ambayo inaundwa na mabilionea ndani ya Yanga. “Kamati hiyo wamewekwa matajiri na wale viongozi waliokuwa wanaunda kamati ya usajili na mashindano ambao ni Seif Magari, Bin Kleb na Davis Mosha ambao waliwahi kuipa ubingwa mara tatu mfululizo kipidi cha aliyekuwa mwenyekiti wa timu, Yusuf Manji.

 

“Hivyo wamerudi tena kivingine ili kuhakikisha wanarejesha heshima Yanga. “Wengine ni mabilionea Rostam na Rais wa Makampuni ya GSM Gharib,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Mshindo Msolla kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Toa comment