The House of Favourite Newspapers

Mkono wa Bwana Kuonekana Tamasha la Vijana Dar, Ijumaa Hii!

KAA mkao wa kula. Tamasha kubwa zaidi la vijana ni Ijumaa hii. Zimebaki takriban siku nne tu. Wakali wa muziki wa Injili Bongo walioko kwenye chati wakiongozwa na Kundi la Zabron Singers ambao wimbo wao wa Mkono wa Bwana ni gumzo kila kona, wanatarajia kulipamba tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika jijini Dar.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Mchungaji Dk Huruma Nkone, amesema tamasha hilo litafanyika kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe jijini Dar na litahudhuriwa na wanamuziki gumzo wa muziki wa Injili.

 

Mchungaji Nkone aliwataja wengine watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo kuwa ni Joel Lwaga, Beda Smith, Walter Chilambo, Students Mass Choir, Rivers of Joy International na wengine kibao.

 

Sambamba na makundi hayo pia kundi maarufu la kudansi nyimbo za Injili la Hype Squad Dancers nalo litaonesha makali yake kwenye tamasha hilo.

Katika tamasha hilo, ukiachilia mbali burudani hizo, faida kubwa kwa vijana watakaohudhuria ni kupata elimu ya kujengwa kiroho na kupewa mbinu za kufanikiwa kimaisha.

 

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo amesema yeye pamoja na walimu wenzake wa uelimishaji na utoaji wa mbinu za kimafanikio, watatoa elimu kwa vijana hao.

 

Shigongo amesema vijana wengine hata wenye elimu ya juu, wanashindwa kufikia mafanikio na kuishia kwenye ufukara kutokana na kukosa elimu ya kiroho.

 

“Unaweza ukakuta kijana ana elimu nzuri, lakini kutokana na mazingira aliyoishi kichwani mwake amejaa roho ya chuki, dhuluma, visasi na kukosa uaminifu, mambo ambayo yanawaangusha vijana wengi hata wakibahatika kupata ajira.

 

“Unakuta kijana ameajiriwa, lakini hana roho ya uaminifu na likibainika hilo, hakuna mahali ambapo atafanikiwa.

“Hivyo elimu ya kiroho ndiyo kila kitu, ninawaomba vijana waje kwa wingi,” alisema Shigongo.

 

Katika tamasha hilo linaloandaliwa na Kanisa la TAG-Victory Christian Centre Tabernacle kwa kushirikiana na Jumuiya za Kikristo na Serikali za wanafunzi wa Vyuo, sasa hivi limeongezewa nguvu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye ameahidi kuimarisha ulinzi na usalama kwa watakaohudhuria tamasha hilo la bure.

 

RICHARD BUKOS, Dar es Salaam

Comments are closed.