The House of Favourite Newspapers

MKUDE APEWA MCHONGO UFARANSA

Jonas Mkude.

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ameshtuka na sasa ameweka wazi kuwa anataka kuondoka klabuni hapo na kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa huku kocha Mzungu akisimamia mchakato wote.

Mkude ni mmoja kati ya viungo tegemeo kikosini humo na amekuwa kwa muda mrefu ndani ya timu lakini sasa anaona wazi kuwa anapaswa kusonga mbele zaidi.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa, mmoja kati ya makocha wa Kizungu waliowahi kuifundisha timu hiyo yupo katika harakati za kumtafutia Mkude timu ya kucheza Ulaya baada ya kuvutiwa na uwezo wake.

 

Habari zinasema kuwa, kocha huyo ambaye Championi linamfahamu lakini liliombwa kutomtaja kwa hofu ya kuvuruga kila kitu, anasuka mpango wa kiungo huyo kwenda kucheza soka la kulipwa huko Ufaransa na ikishindikana basi atakwenda Denmark.

 

Hata hivyo jambo hilo pia linadaiwa kuungwa mkono na

kocha mkuu wa sasa klabuni hapo, Mbelgiji, Patrick Aussems ambaye anataka kumuona Mkude akicheza soka katika moja ya timu kubwa barani Ulaya kutokana uwezo wake.

 

“Mkude anatafutiwa timu Ulaya katika nchi za Ufaransa na Denmark na kocha wetu Mzungu ambaye aliwahi kuifundisha timu hii misimu iliyopita, hata hivyo Aussems naye ameonekana kuunga mkono suala hili kwani anaamini Mkude atafanikiwa kutokana na uwezo wake mzuri uwanjani,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi Jumamosi lilimtafuta Mkude kuzungumzia ishu hii ambapo alikiri na kuongeza: “Ni kweli mchakato huo upo na unafanywa na mmoja kati ya waliowahi kuwa makocha wangu hapa Simba ambaye anaamini kabisa kuwa ninakila sababu ya kucheza soka nje ya nchini.

 

“Kwa hiyo, mambo yakikaa sawa naamini muda wowote naweza kwenda kucheza soka Ulaya, lakini pia naamini uongozi wangu utaniruhusu kama ambavyo ulifanya kwa Mbwana Samatta pamoja na wachezaji wengine wengi,” alisema Mkude.

Stori: Sweetbert Lukonge | Championi Jumamosi

Comments are closed.