The House of Favourite Newspapers

Mkude: Majembe Yaliyosajiliwa Simba ni Hatari

0

Dar es Salaam: SIKU chache baada ya kiungo mkabaji na nahodha wa Simba, Jonas Mkude kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo, ametoa neno zito kwa uongozi wa timu hiyo, huku akipongeza usajili uliofanyika.

Mkude ameongeza mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba hivi karibuni baada ya ule wa awali kufikia tamati na inaelezwa kuwa baada ya kusaini mkataba huo, kwa sasa ndiye mchezaji mzawa mwenye thamani kubwa kuliko wote wanaocheza soka hapa nchini.

Inadaiwa kuwa baada ya kuongeza mkataba huo, alichukua kitita cha Sh milioni 80, lakini pia atakuwa analipwa mshahara wa Sh 5,000,000 (milioni tano) kila mwezi kwa kipindi cha miaka hiyo miwili.

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkude amesema baada ya kufanikiwa kumalizana na Simba, kinachofuata sasa ni kazi tu na hakuna jambo jingine na amewataka Wanasimba kuwa kitu kimoja zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita.

Alisema katika msimu huo ambao Simba ilimaliza kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, alikuwa akikabiliana na changamoto nyingi, na zaidi alikuwa akiumizwa na lawama alizokuwa akitupiwa.

“Nauomba uongozi kuhakikisha unautumia ipasavyo muda huu wa usajili kwa kusajili wachezaji ambao kwa pamoja tutakuwa tukishirikiana nao uwanjani kwa ajili ya mafanikio ya timu yetu.

“Haitapendeza tena kama msimu ujao tutakuwa wasindikizaji tena, Simba wamechoka kusimangwa, wanataka mafanikio, kwa hiyo niwaombe tu hilo walizingatie.

“Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa usajili wote walioufanya mpaka sasa kwani wachezaji wote ni wazuri na wana viwango vya kimataifa, ni matumaini yangu sasa tutapiga kazi kisawasawa,” alisema Mkude.

Simba imefanya usajili wa wachezaji saba mpaka sasa ambao ni Aishi Manula, John Bocco, Shomari Kapombe, Yusuph Mlipili, Jamal Mwambeleko, Emmanuel Mseja na Ally Shomari. Pius Buswita naye inadaiwa amesaini Simba, lakini Yanga nao wanadai wamemsajili na picha zipo.

 

Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI

Leave A Reply