The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu

0

KEVIN Mdoe yuko ndani ya kibanda kidogo kilichojengwa kwa madebe kando ya mto jirani na dampo, ndani ya kibanda hicho, kuna harufu mbaya, ni ya mke wake Catarina, anayeugua kwa muda mrefu, mwili wake umebaki ngozi na nyama na hana fahamu.

Mwanamke huyu amewahi kuwa mrembo kupindukia akishiriki mashindano mbalimbali ya urembo duniani, lakini sasa yupo kitandani! Katika mazingira ya umasikini kabisa, ingawa wote wawili wanatokea familia zenye uwezo mkubwa kifedha.

Nini kilitokea mpaka wakajikuta katika hali hiyo? Kevin anajaribu kukumbuka historia ya maisha yao, alikutana na Catarina wote wakiwa watoto wadogo katika Shule ya Kimataifa ya Academic iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam na wakajikuta wakiishi  jirani.

Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

SONGA NAYO…

ALIKUWA mzuri mno, Kevin pamoja na umri wake mdogo, baba yake akiwa amempa maonyo mengi juu ya kujihusisha na mapenzi kabla ya wakati, alishindwa kabisa kuvumilia! Catarina alimwingia kichwani katika hali ambayo hakuwa na maelezo yake, hakuna siku iliyopita bila kutaka kumwona, walisimama kwenye veranda za nyumba zao na kuongea kila walipotoka shule.

Sauti ya baba yake haikusimama wala kuzimika akilini mwake, maonyo yaliendelea kulia kama muziki kwenye fikra zake, hata hivyo hayakuweza kuondoa hisia alizokuwa nazo kwa Catarina! Lakini mdomo ulikuwa mzito kwake kufunguka na kueleza alivyojisikia, ukizingatia wote wawili walikuwa ni wa umri mdogo.

Kishujaa akaamua kuelekeza akili zake zote kwenye masomo, akiwa ameuahidi moyo wake kwamba angekuwa rafiki mzuri kwa Catarina wala si vinginevyo! Siku zikazidi kusonga, miaka ikazidi kukatika, hatimaye akaingia darasa la saba, yeye na Catarina wakiwa bado marafiki wakubwa, kila siku ya Mungu wakisimama kwenye veranda za nyumba zao na kuongea.

Ilivyokuwa kwa Kevin ndivyo ilivyokuwa moyoni kwa Catarina, alikuwa hoi bin taaban, hisia nzito za kimapenzi zilimsumbua katika umri mdogo, alimpenda Kevin kuliko kawaida lakini kwa jinsi alivyolelewa na wazazi wake walivyomwonya juu ya magonjwa mbalimbali ya zinaa pamoja na mimba za utotoni ambazo zingeweza kuharibu ndoto zake maishani, alishindwa kufungua mdomo wake kumweleza Kevin kilichoendelea moyoni, ukizingatia haukuwa utamaduni wa mwanamke wa Kiafrika kueleza hisia zake kwa mwanaume.

“Nikimwambia mimi ataniona malaya, nasubiri siku atakayosema mwenyewe, nitamkubali lakini hatutafanya tendo la ndoa mpaka tumalize chuo kikuu, pia nitimize ndoto yangu ya kuwa mwanamitindo!” aliwaza Catarina kichwani mwake.

Kila siku waliyosimama kwenye veranda au waliyokutana shuleni, Catarina alitarajia Kevin angefungua mdomo wake na kusema kilichokuwemo moyoni, macho yake yalionyesha jambo, lakini mpaka Kevin anamaliza darasa la saba na kuanza kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya St. Joseph, iliyomilikiwa na Kanisa Katoliki, bado alikuwa hajaweka hisia zake wazi.

Shule ya St. Joseph ilikuwa ni bweni, ikamlazimu Kevin kuondoka nyumbani kwao kwenda shuleni, ilikuwa ni siku ya kuhuzunisha sana alipoagana na Catarina, wote wawili walilia mbele ya wazazi wao, elimu ilikuwa ikiwatenganisha wakati bado walitaka kuendelea kuishi pamoja kama walivyozoea.

“Nitarudi!” Kevin alisema.

“Nitakukumbuka, nitaongea na nani kwenye veranda sasa?”

“Usijali, nitakuwepo moyoni mwako, wewe ni rafiki yangu Catarina, elewa hivyo hata nikiwa mbali na wewe fahamu tu ya kwamba wewe ni rafiki yangu na urafiki wetu ni wa kudumu!”

“Ni urafiki tu?” aliuliza Catarina akijaribu kumrahisishia Kevin azungumze kilichokuwa moyoni mwake.

“Ndiyo!”

“ Hakuna kitu kingine kweli?”

“Kama kipi?”

“Mbona nikikuangalia machoni naona kuna ujumbe!”

“Unayaelewa macho yangu vibaya,” Kevin alijibu wakiwa wamekumbatiana.

Ni kweli alikuwa na ujumbe lakini aibu ilimsumbua, Kevin alikuwa ni aina ya wavulana wenye aibu sana ambaye machoni mwake hakuwahi kumtamkia msichana neno lolote la mapenzi, alitamani afungue mdomo wake na kumweleza “Catarina nakupenda kutoka ndani kabisa ya moyo wangu na ningetaka uwe mke wangu!” Lakini maneno hayo yalishindwa kutoka, ulimi ulinasa kwenye sakafu ya mdomo.

Baada ya Kevin kuondoka nyumbani kwenda St. Joseph na kumwacha Catarina akibubujikwa na machozi na wazazi wake wakihangaika kumtuliza, akiwa hawezi hata kwenda shuleni, walijifunza jambo kuwa mtoto wao alikuwa ameathiriwa na hisia za mapenzi, ili kumsaidia ilikuwa ni lazima wafanye kila kinachowezekana kumtenganisha na Kevin zaidi, ikiwezekana wasionane kwa muda mrefu.

Uamuzi huo ulipofikiwa, baba yake aliamua kumtafutia shule nchini Uganda, akapata shule ya Kikatoliki ya Kampala, Catarina akapewa taarifa hiyo, kwanza aligoma kwani hakufurahia kuondoka Tanzania na kumwacha Kevin, baadaye aliposhawishiwa sana akielezwa hata maneno ya uongo ili tu akubali kuondoka Tanzania, alikubali.

Miezi miwili tu tangu Kevin ajiunge na Shule ya Sekondari ya St. Joseph ambako wanafunzi walibanwa kupita kiasi, hawakuwa na mawasiliano kabisa na nyumbani, Catarina alipanda ndege ya Shirika la Ndege la Uganda na wazazi wake wote wawili hadi Kampala ambako walikodisha gari lililowapeleka moja kwa moja hadi shuleni, alikuwa mtoto kutoka familia yenye uwezo, wazazi wake hawakutaka ateseke kwa lolote.

Akili yote ya Catarina ingawa ilikubali kwenda nchini Uganda ilikuwa kwa Kevin, huo ulikuwa ni mwezi wa kwanza, alitarajiwa kufunga shule mwezi wa sita na kurejea nyumbani kuonana na mtu aliyemwingia moyoni. Shule ya msingi ya Kampala Catholic School, alipokelewa vizuri na walimu pamoja na wanafunzi baada ya wazazi kumkabidhi na kuondoka kurejea Tanzania siku iliyofuata.

Maisha ya shule yakaendelea, mawazo yote yakiwa kwa Kevin, hapakuwa na mawasiliano kati yao, alimuwaza, alimuota usiku mara nyingi na siku zake kuishia kuharibika! Darasani hakuwasikiliza sana walimu, muda wote akili yake ikiwa imefunikwa na taswira za Kevin, akaanza kufanya vibaya darasani tofauti na ilivyokuwa nchini Tanzania.

Ilibidi walimu wafanye udadisi juu ya tatizo lake, kwani alionekana hatilii sana maanani masomo  na afya yake ilizidi kudhoofika, wakawapigia simu wazazi wake kuwajulisha juu ya maendeleo ya mtoto, baba yake akalazimika kusafiri tena kwenda Uganda kumpa mtoto wake nasaha, Catarina alikuwa akilia muda wote wakati akiongea na baba yake.

“Kevin hajambo?”

“Sijawahi kumwona tangu aondoke kwenda shule, yawezekana hawajafunga.”

“Namkumbuka sana baba!”

“Catarina!”

“Bee.”

“Mwanangu soma, huyo Kevin anayesumbua akili yako una uhakika gani kama yeye hivi sasa anakuwazia wewe?”

“Nina uhakika ananiwazia baba.”

“Huwezi kujua, pengine mwenzako anasoma kwa nguvu ili afaulu masomo yake, wewe huku unamlilia, nakusihi uachane na hayo mawazo, usome mwanangu wakati mimi nina uwezo wa kukusomesha!”

“Siwezi baba nashindwa!”

“Jitahidi.”

Akili ya Catarina haikuwa sawa, akauomba uongozi wa shule amchukue kumpeleka kwenye maombi kwa Mtumishi wa Mungu maarufu nchini Uganda, Nabii Moses Sebagerere, aliyeaminika kwa kutenda miujiza kupitia neno la Mungu, kichwani mwake baba yake alidhani pengine mwanaye alikuwa ametupiwa mapepo ili maisha yake ya baadaye yaharibike.

Maombi yalifanyika ofisini kwa nabii huyo  lakini Catarina hakuonyesha dalili yoyote ya kuwa na pepo, ikabidi arejeshwe shuleni  na kukabidhiwa kwa walimu saa kumi na moja jioni. Kwa wiki nzima baba yake alikuwa jijini Kampala akijaribu kumtuliza mpaka alipoonyesha nafuu kidogo ndipo akaondoka kurejea Tanzania.

Mwezi Juni ulipofika, shule ilifungwa, Catarina akakatiwa tiketi ya ndege na kurejea jijini Dar es Salaam, kitu cha kwanza alichokifanya baada ya kuingia ndani ya nyumba yao ni kukimbia moja kwa moja hadi kwenye veranda na kutupa macho yake kwenye veranda ya akina Kevin, hakumwona!

“Kevin! Kevin!” akaita kwa sauti ya juu.

Mlango ukafunguliwa na baba yake Kevin akatokeza nje uso wake ukiwa umejawa na tabasamu na kuanza kuongea na Catarina akimweleza kuwa Kevin alikuwa bado yuko shuleni, wao walitarajiwa kufunga mwezi wa saba katikati. Catarina akaonyesha masikitiko yake baada ya kupewa kauli hiyo.

“Hajambo lakini?”

“Hajambo, huwa anakuulizia kila mara ninapokwenda shuleni kumwona.”

“Anaendeleaje na shule?”

“Anaendelea vizuri, fikra juu yako bado zinamtesa, ilibidi mpaka tumtafutie wataalam wa saikolojia kumweka sawa, alikuwa akikuwaza sana mpaka masomo yakaanza kumshinda.”

“Mungu wangu!” Catarina alisema maneno hayo machozi yakianza kumbubujika.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply