The House of Favourite Newspapers

Mkuki Moyoni Mwangu 055

0

ILIPOISHIA…

 

KWA kutumia washirika wake waliobaki nje, Jackson Motown anafanya kila kinachowezekana ili kuhakikisha Catarina anakufa ili kupoteza ushahidi wote kwani hayuko tayari kuingia mikononi mwa sheria. Anamtumia Dracula ili kukamilisha mpango huo akimuahidi kiasi kikubwa cha fedha.

Dracula anapanga mpango mzima kwa kushirikiana na Ofisa wa FBI ambaye ni kibaraka wao ili kukamilisha zoezi hilo. Anaingia nyumbani kwa Catarina kama Padri Coronel Garsia kukiwa hakuna hata mtu mmoja, si FBI wala wazazi wa Catarina anayemshtukia. Huko anajifanya mtoa nasaha ili kumfanya Catarina apone na kurejea katika hali ya kawaida.

Je, nini kitaendelea? Atafanikiwa na mpango wake huo?

 

SONGA NAYO…

U

PELELEZI ulipokamilika, kesi ya Jackson Motown na wenzake ilianza kusikilizwa, upande wa mashtaka ukawasilisha mbele ya jaji kesi ya kubaka na ya mauaji ya watu saba! Jackson ambaye katika kesi hiyo alikuwa na watu wengine wanne, akiwemo mlinzi wake Dragon, walikanusha mashtaka yote.

Mawakili wao wakajipanga kwa ajili ya utetezi wakiwa na uhakika kabisa kusingekuwa na shahidi yeyote ambaye angesimama mahakamani na kusema alikuwa na uthibitisho kuwa Jackson Motown alibaka kwa kushirikiana na wenzake kufanya mauaji ili kuficha ushahidi.

Watu wawili tu walionekana ni chumvi kwenye kidonda, hawa walikuwa ni Catarina na Mariana, kwa amri ya Jackson Motown kwa Dracula ambaye aliendeleza mauaji yote nje ya mahabusu, ilikuwa ni lazima wauawe kabla kesi haijatajwa tena mahakamani mwezi mmoja baadaye.

Wiki mbili tu baadaye, Mariana alikutwa amekufa bafuni kwake, sindano ikiwa kwenye mshipa wake wa damu kuashiria kwamba alijidunga kiasi kikubwa cha dawa ya kulevya aina ya heroine! Mwili wake ulikuwa umeharibika vibaya, ikiwa ni dalili kuwa alikufa siku chache kabla ya kugundulika.

Mazishi yake yakafanyika kimyakimya na baada ya hapo hapakuwa na uchunguzi  wala upelelezi wowote uliofanyika, kila mtu akisema “dawa za kulevya ndizo zilizomuua!” bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia ambako Jackson Motown na washirika wake walihusika asilimia mia moja na kifo hicho.

Kazi ngumu ilionekana ni kumuua Catarina, ambayo Dracula ama Padri Coronel Garsia kama alivyojulikana kwa FBI alitaka kuifanya mwenyewe bila mtu yeyote kushtuka ama kuacha alama nyuma ambayo ingesababisha kukamatwa kwake na kufikishwa mbele ya sheria na hatimaye kuhukumiwa kifo, alitaka afanye mauaji ya Catarina kwa akili nyingi sana, baada ya hapo abaki huru akifaidi malipo ambayo Jackson Motown aliahidi kumlipa.

Walichagua kumuua Catarina  katika tukio ambalo lingeonekana ni ajali wakishirikiana na Clarence Nicolaus Ofisa wa FBI aliyekuwa upande wao, hatua ya kwanza ya zoezi hilo ilikuwa  ni kuendelea kwa Padri Coronel kwenda mahali alikofichwa Catarina kumpa nasaha na huduma za kiroho, badala ya kwenda mara moja kwa wiki akawa anakwenda mara mbili hatimaye akazoeleka kabisa, askari wa FBI wakawa hawana sababu tena ya kumfunga kitambaa usoni baada ya kujenga imani kwamba asingeweza kusaliti sababu alikuwa ni Mtumishi wa Mungu.

Hilo ndilo kosa walilolifanya, Dracula ambaye pia alishazoeana sana na Catarina, akaitumia nafasi hiyo kumshawishi akamtembeze mjini jioni ya siku iliyofuata sababu akili yake ilishatulia, kisaikolojia alikuwa sawasawa! Catarina hakuona sababu ya kukataa, alipoongea na Ofisa wa FBI Clarence, aliyekuwa ndani ya mpango wa mauaji hayo, alikubaliwa, Catarina badala ya kusikitika, akiwa hajui kilichokuwa kimepangwa kutokea, alifurahi mno.

Siku iliyofuata saa moja na nusu usiku, waliingia ndani ya gari la FBI aina ya Ford, wakiwa watatu, kwenye usukani akiwa Clarence, Catarina aliketi kwanza kiti cha nyuma lakini Padri Coronel akamlazimisha aketi kiti cha mbele, yeye ndiye akaketi nyuma peke yake.

“Baba na mama nitawakuta baada ya muda mfupi!”

“Hakuna shida!” waliitikia, hakuna aliyekuwa na wasiwasi wowote, laiti wangefahamu ambacho kingempata mtoto wao wasingeruhusu aondoke.

Catarina alikuwa mwenye furaha, maneno ambayo Padri Coronel alimwambia kwenye ushauri nasaha tangu wakutane yalikuwa yamemjenga upya, fikra nyingi juu ya Kevin zilishapungua kwa kiasi kikubwa. Waliongea mengi ndani ya gari, saa mbili baadaye wakaingia katikati ya jiji na kuendelea hadi upande wa pili ambako walizidi kusonga mbele kwa kasi wakipandisha kilima kirefu.

Saa ya mkononi ya Catarina ilisomeka saa nne kamili, safari ilikuwa bado ikiendelea kupandisha kilimani ambako wala hawakukutana na binadamu wala gari yoyote! Wasiwasi ukaanza kumwingia Catarina, kitu fulani kikaanza kumwambia moyoni kuwa jambo lisilo la kawaida lilikuwa mbioni kutokea.

“Why are we not reaching a destination?”(Kwa nini hatufiki mwisho?)

“Soon we will be there!”(Tutafika sasa hivi!)

“No! Let’s turn back, I have had enough of a tour!”(Hapana! Turudini, safari tuliyozunguka imetosha!)

“No! Let’s go to the mountain top!”(Hapana! Twende kileleni!)

“It is getting darker!”(Giza linazidi kuongezeka!)

“Don’t worry, you are here with me!”(Usiogope, uko hapa na mimi!) Ofisa wa FBI alijibu na kumfanya Catarina atulie, hofu ikaondoka, asingeweza kufanyiwa ubaya wowote afisa huyo akiwepo.

“Are you sure I am safe?”(Una uhakika niko salama?)

“One hundred percent!” (Asilimia mia moja!)

“Stop! Stop! I want to urinate!”(Simama! Simama! Nataka kujisaidia haja ndogo!)  Dracula aliongea na Clarence akakanyaga breki ya gari na ikasimama.

Haraka akashuka na kuzunguka nyuma ya gari ambako badala ya kujisaidia alichomoa simu yake mfukoni na kupiga namba ya simu aliyoifahamu yeye kisha kuanza kuongea kwa sauti ya kunong’ona kwa sauti ya chini akiwa makini mtu yeyote aliyemo ndani ya gari asisikie.

“Get ready!” (Kaeni tayari!)

“Where are you?” (mko wapi?) sauti upande wa pili ilisikika sikioni mwake.

“One hundred meters from the corner!” (Mita mia moja kutoka kwenye kona!)

“We are more than ready, just bring her to meet her death!”(Tuko zaidi ya kuwa tayari, ninyi mleteni tu akutane na kifo chake!)

“Few seconds!” (Sekunde chache!) alisema Dracula na kuzima simu kisha kurejea kwenye gari na safari ikaendelea kichwani mwake akifikiria mauaji ya Catarina ambayo walikubaliana kumuua kisha kuligonganisha gari na katapila maiti ya Catarina ikiwa ndani yake ili ionekane kuwa gari hilo liligongana na Katapila upande wa mbele ya abiria.

 

Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply