Mkuki Moyoni Mwangu 32
KEVIN amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku mpenzi wake wa tangu utotoni Catarina, amekomea kidato cha nne na kuondoka kwenda Afrika Kusini kujishughulisha na masuala ya mitindo, lengo lake ni kuwa mwanamitindo maarufu duniani na sifa anazo kwani kujitokeza kwake tu, kumeitingisha dunia nzima ya mitindo.
Ahadi ya wawili hawa ni kutunza bikira zao mpaka watakapofunga ndoa, wasiwasi wa Kevin ni maisha ya uanamitindo, hasa kwa sababu anaufahamu vizuri urembo wa mpenzi wake! Ahadi ya Catarina ni kujitunza na kuepuka vishawishi ambavyo vingeambatana na kazi yake mpaka watakapooana.
Mambo yanakuwa tofauti nchini Afrika Kusini ambako amekutana na Jackson Motown, bilionea kijana wa mambo ya mitandao ambaye amemtaka kimapenzi kwa lengo la kumuoa lakini Catarina amekataa, Motown anaahidi kutumia uwezo wake wote mpaka Catarina awe mke wake.
Miezi michache baadaye, Catarina anakaribishwa chakula cha usiku na wakala wake Craig Anderson, huko anashawishiwa kunywa pombe na baadaye kulewa kabisa kiasi cha kupoteza fahamu, alipozinduka asubuhi alijikuta kitandani na Motown, mashuka yakiwa yamelowa damu, bikira yake imepotea.
Anamchukia Craig kwa kumuuza kwa Motown, wiki mbili baadaye wanaondoka kwenda Ufaransa kwenye maonyesho ya mavazi ya Paris, Catarina akiwa bado ana chuki dhidi ya Craig! Anakutana na Mario Pizaro, mbunifu wa mitindo bilionea ambaye anamshawishi waende wote New York, huko angemtafutia kampuni nyingine ya kufanya nayo kazi na Catarina anakubali na kuacha kazi Fonex Modelling.
Ndege binafsi waliyopanda, ya tajiri ambaye Catarina ameambiwa angemwajiri kwenye kampuni yake ikiwa angani, anapewa taarifa kuwa tajiri huyo angemfuata chumbani kwake kwa maongezi, alipokuja dakika tano baadaye, Catarina hakutaka kuyaamini macho yake alipomshuhudia Jackson Motown tena akiwa mtupu.Je, nini kiliendelea?SONGA NAYO…
MWILI wote wa Catarina ulikuwa ukitetemeka, kama vile mtu aliyenyeshewa na mvua kwa muda mrefu. Hofu kubwa ilikuwa imeugubika moyo wake, mwanzo alihisi ni ndoto, maana ilikuwa haiwezekani kwa fikra za kawaida kuamini kuwa kwa mara nyingine tena alikuwa mikononi mwa baradhuri, mtu aliyetumia utajiri wake kumnyanyasa kingono; Jackson Motown.
Machozi yalikuwa yakitiririka kwa kasi kupitia mbele ya uso wake kukatisha mashavuni kuelekea shingoni, hasira aliyokuwa nayo haikuwa na maelezo, akaangalia huku na kule chumbani kuona kama kulikuwa na kitu angeweza kukitumia kujilinda, hapakuwa na chochote isipokuwa kiatu chake kirefu, chenye kisigino ambacho kwa chini kilikuwa na chuma.
“Ha! Ha! Haaa! I told you, it is impossible to run away from me, whether you like it or not, one day you gonna be my wife, the only thing you are going to do today is to make the young billionaire Jackson Motown feel good!” (Ha! Ha! Haaa! Nilikuambia, haiwezekani kunikimbia, utake usitake siku moja utakuwa mke wangu, lakini kwa leo utakachofanya ni kumfanya Jackson Motown, bilionea kijana, ajisikie raha!)
“Never! Never again! If you dare touch me, your face will be destroyed!” (Kamwe! Haitatokea tena! Kama ukithubutu kunigusa, uso wako utaharibiwa!)
“Who will destroy my face?” (Nani ataharibu uso wangu?)
“Me!” (mimi!)
“Do you know who is Jackson Motown?” (Hivi unajua Jackson Motown ni nani?)
“I don’t care who the hell is Jackson Motown, what you did to me in South Africa won’t happen here! You son of a bitch who use money to discriminate women.” (Sijali Jackson Motown ni nani, ulichonitendea huko Afrika Kusini hakiwezi kutokea tena hapa, mtoto wa malaya wewe unayetumia fedha zako kuwanyanyasa wanawake!) alifoka Catarina.
Jackson Motown alibaki kimya akimtazama Catarina aliyekuwa ameketi kitandani, macho yamemtoka, mkononi akiwa ameshikilia kiatu chake chenye kisigino cha chuma, taswira yake ilionyesha alikuwa hatanii, alichosema ndicho angefanya, hofu ikamwingia kidogo Jackson Motown, akarudi kinyumenyume na kufungua mlango, badala ya kutoka akaishia kuchungulia.
“Dragon!” Akaita.
“Yes boss!” (Ndiyo mkuu!)
“Come in here, this bitch is calling me bad names!” (Ingia, huyu malaya ananiita majina mabaya!)
Mtu wa miraba minne, mrefu aliyejaza vizuri sababu ya mazoezi, ambaye kwa kumwangalia mara moja alifanana kabisa na raia wa Mexico akaingia na kusimama katikati ya chumba akimwangalia Catarina huku akisubiri maelekezo kutoka kwa Motown.
“Undress her!” (Mvulishe!)
***
Ilikuwa ni katikati ya usiku majira ya saa saba, miungurumo mizito ilikuwa ikisikika angani na miale ya radi ikimulika mpaka ndani ya chumba alicholala Kevin, hiyo ndiyo iliyomzindua kutoka usingizini, akaketi kitako katika mshtuko akiwa katikati ya giza nene, sababu umeme ulikuwa umekatika huku mvua kubwa iliyoonekana kuwa ya mawe ikinyesha kwa nje.
Usingizi uligoma kabisa baada ya hapo, mawazo yake yote yakaelekea sehemu moja tu; kwa Catarina, msichana aliyempenda kupindukia. Siku nzima kabla alikuwa amempigia simu bila mafanikio, moyoni mwake akaelewa ni kwa sababu ya shughuli nzito ya kuonyesha mavazi aliyokuwa nayo siku hiyo kwenye Jiji la Paris.
Maisha yake yalikuwa magumu sana baada ya Catarina kuondoka nchini Tanzania yeye akijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, haikupita siku bila kumfikiria, mara zote akimwombea kwa Mungu afanikiwe alichokwenda kukifanya ili baadaye maishani waungane pamoja na kuishi maisha ya mafanikio.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilikuwa na sifa ya kuwa na wasichana warembo kuliko vyuo vingine vyote nchini Tanzania, Kevin alipojiunga nacho tu mwaka wa kwanza alichaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi iliyoitwa DARUSO, pia akawa mchezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya chuo ambako alifanya vizuri sana kiasi cha jina lake kuvuma.
Kanisani kwao alikuwa mpiga kinanda wa kwaya ya kusifu na kuabudu, kazi ambayo ilimfanya ang’are sana kanisani na kuwa tegemeo la kwaya. Kote huko kuanzia chuoni, kwenye uwanja wa mpira wa kikapu, kanisani, Kevin aliwavutia wasichana wengi. Kama kulikuwa na usumbufu mkubwa alioupata basi ulitoka kwa watoto wa kike.
Kilichowachanganya zaidi wasichana pia kilikuwa ni umbile lake, Kevin alikuwa mrefu, mwenye mwili uliojengeka sababu ya kufanya sana mazoezi na alijua kuvaa vizuri huku akipendelea kunukia manukato kila siku, bila kufahamu kwa kufanya hivyo aliwavuta wasichana wengi kumwelekea kama vile ambavyo nyuki hufuata maua.
Pamoja na vishawishi vyote vya wasichana, Kevin alisimama imara, hakuwa tayari kumsaliti Catarina wake, mwanamke pekee aliyempenda kuliko wengine wote duniani isipokuwa mama yake mzazi. Ahadi waliyopeana ya kutokutana na mwanaume au mwanamke kimapenzi mpaka siku ya ndoa, ilikuwa kichwani mwake, asingeweza kuenenda kinyume na alichomuahidi Catarina.
“Alikuwa bize sana jana bila shaka, nitajaribu kumpigia tena asubuhi, ikishindikana nitawapigia wazazi wake nijue kama waliongea naye!” aliwaza.
Saa mbili baadaye alipitiwa na usingizi, alipozinduka ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu, siku hiyo hakuwa na kipindi cha asubuhi, hivyo akaendelea kulala mpaka saa tatu kamili ndipo akainuka. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumpigia Catarina, simu ilikuwa imezimwa.
Mara moja akapiga simu ya mama yake Catarina na kufanikiwa kumpata, habari alizopewa zilimshtua na kumfanya ashangae ni kwa nini Catarina hakumwambia mwenyewe juu ya safari yake ya kwenda New York baada ya kupata kampuni nyingine ya kufanya nayo kazi za uanamitindo.
“Kwa hiyo amekwenda New York?”
“Ndiyo mwanangu!”
“Nimefurahi sana!”
“Hata sisi pia tumefurahi mno!”
“Ametimiza tulichoahidiana, kwamba siku moja atahamia New York na mimi nitamfuata.”
“Ni kweli, hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake, alisema akitua tu New York atatupigia simu!”
“Na mimi mtanipatia namba yake!”
“Tutafanya hivyo!”
“Ahsante mama, siku njema, msalimie sana baba!”
“Nashukuru!”
Jambo ambalo wote hawakulifahamu ni kwamba Catarina alikuwa katika shida kubwa ndani ya ndege kubwa ya Jackson Motown, laiti wangefahamu mambo yaliyokuwa yakimkuta, wote wangebubujikwa na machozi.
Je, nini kilimpata Catarina ndani ya ndege? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1