Mkumbo utakavyowagharimu vijana miaka 5 ijayo

SHABIKIA SIASAKatika michakato yote ya chaguzi zilizopita, mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu, unatajwa kuwa wa kipekee zaidi kutokana na kuwepo kwa mwamko mkubwa wa watu wengi wa kada mbalimbali huku vijana wakiwa kundi kubwa la watu waliojitokeza kuliko makundi yote.

SHABIKIA SIASAANdani ya kundi hilo la vijana wapo wafanyakazi wa serikali na wenye ajira binafsi kama vile waendesha bodaboda, wafanyakazi wa viwandani, wafanyabiashara, wakulima na wachimba madini huku wengine wakiwa wale ambao hawapo kwenye ajira kama vile wasomi, wakaa vijiweni na wengine wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile ukabaji na matumizi ya madawa ya kulevya.

Wote hawa wanaunda kundi moja kubwa la vijana na kwa mwaka huu wa uchaguzi kama nilivyosema awali; vijana wameamka na kuamka huko kunaashiria kuwa ushiriki wao katika hatua muhimu ya kupiga kura pia ni mkubwa zaidi kuliko miaka iliyopita na pengine wanaweza wakazidi makundi mengine kwa idadi yao.

Wanasiasa nao wameshtukia jambo hilo, na wanawatumia vijana hao kama rasilimali pekee ili kuhakikisha wanawapigia kura na kuhamasisha makundi mengine kama akina mama na wazee ili kuwapa chapuo wao kwenye nafasi wanazogombea.

Si kosa kwa wanasiasa kufanya hivi lakini hofu yangu ni juu ya vijana ambao hawajali kusikiliza wala kupambanua sera za wagombea kumezwa na vuguvugu la mkumbo wa ‘tumchague fulani’ ambalo huwachota vijana kirahisi kwa kuwa sifa ya kufuata mkumbo ni tabia ya vijana kote duniani.

Turudi kwenye kile ambacho nimepanga kukizungumzia; binafsi nawatazama vijana kama nguvu kazi ya taifa, watu wenye malengo kimaisha, lakini pia nawatazama kama kundi la watu wanaopigana kutwa kucha kujenga msingi wa maisha yao ya sasa na yajayo.

Kuna vijana ambao wameanza maisha baada ya kumaliza masomo yao, pia kuna kundi kubwa la vijana ambao wana malengo ya kujiajiri ama kuajiriwa kwenye sekta mbalimbali nchini. Kama hiyo haitoshi kuna kundi jingine la vijana ambao wanaendelea na elimu yao na wengine wanatumia vipaji vyao kusonga mbele kimaisha.

Haitoshi, kuna kundi kubwa la vijana ambao kutokana na umaskini, wamekuwa wakitegemewa na familia na wazazi wao hivyo wana mzigo mkubwa wa kufanya kazi na pengine tumaini lao la maisha bora kwa miaka mitano ijayo wameliweka kwa mgombea anayepiga kampeni jukwaani sasa.

Vijana hao ndiyo ambao ukiwaangalia kwa mtazamo wangu, utagundua kuwa ndiyo waathirika wakubwa wa matokeo ya viongozi wabovu serikalini baada ya kuwachagua.

Maana yangu ni kwamba viongozi ambao vijana wanawachagua watutumikie kwa miaka mitano ijayo ndiyo hubeba mustakabali wa maisha ya kimaendeleo ya vijana hao kwa miaka mitano ijayo, kwa kuwa wanaweza wakafanya kijana akatimiza malengo yake au akashindwa kuyafikia wakati huohuo umri ukizidi kusonga na kumtupa kijana wa leo kwenye kundi la wazee wa kesho ambao nguvu zao za kufikiri na uzalishaji ni ndogo.

Najua hakuna kijana ambaye anataka kubakia palepale kwa miaka mitano ijayo kwa kumweka mtu ambaye anajua fika hakumchagua kwa matakwa yake bali kwa msukumo kutoka kwa wenzake.

Nafahamu pia kuna wengi ambao wanalia kwa kukosa ajira na lawama unapewa uongozi uliokuwa madarakani, lakini unaweza ukajitendea haki mwenyewe kwa kujiuliza je, katika uongozi huohuo unaotupiwa lawama hakuna watu waliofanikiwa? Na kama uongozi mpya utachaguliwa je, ndiyo ajira zitapatikana kwako na kwa kila mtu?

Wapo ambao wanabeza mafanikio ya uongozi uliopita wakitarajia mafanikio kwa uongozi ujao kwa kubadilisha mrengo wa vyama vya kisiasa bila kujali nani wanayemchagua, lakini hata hivyo kijana anatakiwa ajiulize kuwa huyo anayemchagua amuongoze ana uwezo wa dhati wa kufanya hivyo au yupo kwa ajili ya kutimiza ndoto zake za kuwa kiongozi?

Lengo langu siyo kumfanya kijana awe na mtazamo usiokubali mabadiliko bali ni kumjengea uwezo binafsi wa kutambua maamuzi yake mwenyewe bila kufungwa na mkumbo. Kuanzia hapo ndiyo mtu anaweza kumchagua mtu mchapakazi bila kujali chama anachotokea mtu huyo kwa kuwa upofu wa mkumbo anakuwa hanao.

Nataka niwaambie vijana kuwa wakati makundi ya akina mama na wazee wakiuona uchaguzi huu kama uchaguzi tu, vijana wauone uchaguzi huu kama karata yao ya mwisho kabla ya kuelekea uzeeni ambapo wanatakiwa waicheze kwa umakini mkubwa bila kufuata ushabiki wala mkumbo ili wasije kujutia uamuzi wao maana umri nao hausubiri.


Loading...

Toa comment