The House of Favourite Newspapers

Mkurugenzi Manispaa ya Kigamboni Awaondoa Hofu Wakazi wa Mikenge

0
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigamboni, Erasto Kiwale.

 

 

BAADA ya zaidia ya miaka saba ya mgogoro wa barabara kati ya wananchi na mwekezaji kampuni ya ASM (T) LTD katika mtaa wa Mikenge kata ya Kimbiji Manispaa ya Kigamboni, hatimaye Halmashauri ya Wilaya hiyo imesema ipo mbioni kuumaliza mgogoro huo.

 

Mgogoro huo uliibuka baada ya mwekezaji ASM (T) LTD kufunga barabara inayopita kwenye viwanja vyake kwenda maeneo mengine ya wawekezaji na Pwani ya bahari na kuleta mvutano wa muda mrefu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigamboni, Erasto Kiwale, alisema baada ya maagizo kutoka ngazi za juu na vikao mbalimbali vya kumaliza mgogoro huo, tayari taratibu za kiofisi zinaendelea ili kumlipa fidia mwekezaji huyo na kuvunja ukuta alioujenga kupisha barabara hiyo kutumika.

 

Alisema kwa sasa taratibu za kiofisi zinaendelea kwa kuwa suala la ulipaji wa fidia ni mchakato unaohusisha wataalam mbalimbali.

 

“Niwaombe tu wananchi na wawekezaji wa maeneo yale kuwa wavumilivu wakati suala ili likiendelea kufanyiwa kazi ndani ya ofisi, tunafahamu ni mgogoro wa muda mrefu na sasa tumefika suala la ulipaji fidia, huu ni mchakato ambao kuna wataalamu mbalimbali wanahusishwa kabla ya ulipaji wenyewe na kulichukua lile eneo,” alisema Kiwale.

 

Aidha, alisema Serikali ipo kwa ajili ya wananchi hivyo kero na shida za wananchi zinapewa uzito mkubwa.

 

“Lakini pia Serikali inawahitaji wawekezaji, tunachofanya ni kuweka mazingira mazuri ya Uwekezaji ili anayewekeza apate kile alichokikusudia na Serikali pia ipate kinachostahili huku wananchi nao wakiendelea na shughuli zao kwa amani,” alisema Kiwale.

 

Pia, alikiri kuwa tathimini ya awali katika eneo hilo lililofungwa barabara imefanyika kwa  sasa taratibu nyingine zinaendelea ili kulikamalisha jambo hilo.

 

“Ulipaji fidia ni mchakato wa kisheria na lazima ukamilike, kilichofanyika pale ni uthamini wa awali na hatua nyingine zimeshaanza, tunaamini tutalimaliza hili mapema,” alisema Kiwale.

 

Alisema kama Manispaa wanataka kuona wawekezaji wengine katika maeneo hayo ya fukwe wanapata uwezo wa kufika kwenye maeneo yao na kuendelea na biashara zao.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mikenge, Lameck Mayala, alisema wanaiomba Serikali kumaliza mapema mgogoro huo ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na shuguli zao kupitia barabara hiyo iliyofungwa. Alisema mgogoro huo ni wa wa muda mrefu na umepelekea shughuli nyingi za kiuchumi kusimama.

 

“Hii barabara ndio iliyokuwa inatumiwa na wananchi kufika baharini kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa sababu wakazi wengi wa huku wengi ni wavuvi na hii ndio barabara iliyokuwa inawafikisha baharini, lakini ukiondoa wananchi ukipita viwanja vya mwekezaji ASM, mbele kuna wawekezaji wengine wamejenga hoteli zaidi ya nne na vijana wetu wengi walipata ajira huko, kwa sasa hoteli zimefungwa na watoto wetu wengi wamepoteza ajira,  tunaomba Serikali kwa sababu tayari wamekiri kuufanyia kazi, basi mchakato uharakishwe jambo ili liishe,” alisema Mayala.

 

Aidha, mmoja wa wekezaji wa hoteli katika maeneo hayo, Vidate Msoka, ameiomba Manispaa kuharakisha kumaliza mgogoro huo ili barabara hiyo ifunguliwe na waendelee na biashara zao.

 

“Kwa sasa hakuna kinachoendelea, biashara zimesimama tulilazimika kuwaondoa watu kazini kwa sababu hakuna wageni wanaokuja kutokana na kufungwa kwa barabara hii, tunaomba mchakato huu uharakishwe kwa sababu ni mgogoro wa muda mrefu,” alisema Vidate.

 

Pia mwekezaji mwingine, Arif Sheikh, alisema wanashukuru kwa hatua ambayo Manispaa ya Kigamboni imechukua lakini anaomba kuharakishwa mchakato wa kumlipa fidia mwekezaji huyo aliyefunga barabara.

 

“Huu mgogoro ni wa muda mrefu sana, vikao vingi vimefanyika na mpaka kwa muheshimiwa Waziri Anjelina Mabula (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi) umefika, sasa kwa sababu kwa sasa upo kwenye hatua ya kumlipa fidia huyu mwekezaji, basi tunaomba mchakato wake ukamilishwe mapema ili na sisi tuendelee na biashara zetu, tumelazimika kufunga hoteli na huku kuna hoteli si chini ya nne za wawekezaji tofauti tofauti, zote zimefungwa kwa kukosa barabara,” alisema Sheikh.

 

Mgogoro huo wa barabara uliibuka baada ya mwekezaji ASM anayemiliki viwanja viwili pacha kwenye eneo hilo la Mikenge kupinga kuwepo kwa barabara iliyopita katikati ya viwanja hivyo na kuvitenganisha.

Leave A Reply