The House of Favourite Newspapers

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Wiki ya Huduma Kwa Wateja Inatukumbusha Wajibu wa Kutoa Huduma Bora

0


Wiki hii, makao makuu ya PSSSF yamezindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja, tukio ambalo linatarajiwa kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wanachama na wadau wengine.
Akizungumza na watumishi wa makao makuu na kanda ya Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru, alieleza kwamba wiki hii ni fursa ya kutafakari jinsi wanavyotoa huduma.
“Ukimhudumia mwanachama vizuri unakuwa uneenda above and beyond, na hii ndio theme inayotuongoza,” aliongeza.


Akisisitiza umuhimu wa wiki hii alisema, “Wiki hii ni muhimu sana kwani inatukumbusha kwa nini sisi watumishi tupo hapa. Wateja wetu ndio wanaotufanya sisi kuwa hapa kazini kwa lugha ya mjini wanasema ndio wanaotufanya tuwepo mjini.” Alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma katika mazingira yote na kwa wateja wa aina zote. “Wiki hii inatukumbusha majukumu yetu kama mfuko, ambayo ni kuhakikisha kuwa fedha ya wanachama inakuwa salama na inapata thamani zaidi. Tunatarajia kwamba pale wanapolipwa fedha yao iwe na thamani,” alifafanua.

Badru alisisitiza kwamba PSSSF inatoa ahadi upya kwamba wana uwezo wa kutoa huduma bora na kuwafanya wateja wao kuwa na furaha na kuridhika. “Theme hii ya mwaka huu ni ‘Above and Beyond’ – Kutoa huduma kwa wateja wa aina zote, umri wote na jinsia zote, na kuwa na uwezo wa kuwaelewa na kuwasikiliza wateja wetu,” alisema.
Aliwashukuru watumishi wote kwa juhudi zao katika kutoa huduma bora na kutangaza kuwa wako tayari kutoa huduma kwa viwango vya juu zaidi na kutoa suluhisho kwa mahitaji na changamoto za wateja wao.
Alimalizia hotuba yake kwa kusema, “Katika kutoa huduma, ni lazima kutoa huduma kwa tabasamu, yaani ‘corporate smile’. Tabasamu ni ishara ya ukaribu na urafiki, na linachangia kwa kiasi kikubwa katika kuridhisha wateja wetu.”
Wiki ya Huduma kwa Wateja inatarajiwa kuendelea kutoa mwanga kuhusu majukumu ya kila mfanyakazi na kuimarisha uhusiano kati ya PSSSF na wanachama wake.

Leave A Reply