The House of Favourite Newspapers

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Aomba Menejimenti ya TAEC Kumpa Ushirikiano

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed  ameitaka menejimenti ya TAEC pamoja na wafanyakazi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kuongoza taasisi hiyo yenye dhamana ya kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini sambamba na  kuendeleza teknolojia ya nyuklia.

Prof. Najat  ameyasema hayo wakati akikabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Prof. Lazaro  Busagala, ambapo makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya menejimenti ya TAEC, Makao Makuu eneo la Kikombo Jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Prof. Najat Kassim Mohammed amewataka wafanyakazi na menejimenti kumpa ushirikiano ili kuhakikisha majukumu ya taasisi hiyo yanatekelezwa kwa maslahi ya taifa la Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAEC aliyemaliza muda wake Prof. Lazaro Busagala  amemtakia kazi njema Mkurugenzi Mkuu Prof. Najat  na kuwasihi wafanyakazi wa TAEC kushirikiana katika kuhakikisha gurudumu la maendeleo linasonga mbele.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wote wa TAEC Mkurugenzi wa kitengo cha udhibiti wa mionzi Dkt. Justine Ngaile  amemkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Prof. Najat Kassim Mohammed na kumuahidi ushirikiano huku akimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TAEC aliyemaliza muda wake Prof. Lazaro Busagala  kwa utumishi wake ndani ya taasisi hiyo.