The House of Favourite Newspapers

Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal Atimka Klabuni

Klabu ya Arsenal imetangaza rasmi kuondoka kwa mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo, Ivan Gazidis aliyetimkia AC Milan ya Italia katika nafasi hiyo hiyo.

 

Gazidis ambaye alijiunga na Arsenal, Januari 2009 alikuwa akihusishwa na tetesi za kuihama klabu hiyo tangu mwanzoni mwa mwezi huu pamoja na kauli ya kocha, Unai Emery ambaye alikiri kutofahamu hatma ya kiongozi huyo.

 

Akinukuliwa katika tovuti ya klabu ya Arsenal, Gazidis amesema; “Kwa zaidi ya miaka 10 nimejizatiti kuwepo katika klabu hii kubwa. Arsenal inaingia katika ukurasa mwingine na nimefanya kila kitu kuhakikisha kuwa inafikia katika hatua hiyo ikiwemo vifaa vyenye hadhi ya kimataifa pamoja na kuwaleta viongozi wazuri ”.

 

“Sasa ninajiandaa kujiunga na moja ya klabu kubwa duniani, AC Milan ambayo nitafanya kazi kuirejesha katika nafasi yake sahihi ya soka, nina furaha na amani kwa yale yajayo mbele yangu na kwa Arsenal, na Arsenal itakuwa moyoni mwangu daima ”, Ameongeza, Gazidis.

 

Mkurugenzi huyo aliiongoza Arsenal katika mchakato wa kumpata kocha, Unai Emery baada ya kuondoka kwa Arsene Wenger ambaye aliachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuiongoza kwa miaka 22.

 

Viongozi wawili wameteuliwa kuchukua nafasi hiyo iliyoachwa na Gazidis, ambao  ni Raul Sanllehi pamoja na Vinai Venkatesham.

 

Nao viongozi wakuu wa klabu ya Arsenal wakiongozwa na Mwenyekiti wa klabu, Sir Chips Keswick amesema Arsenal imejivunia kufanya kazi na kiongozi huyo ambaye ameiongoza kwa ubunifu mkubwa na ameiacha katika sehemu nzuri, akimtakia mafanikio mema katika klabu mpya anayokwenda.

Comments are closed.