MKUTANO wa 39 wa wakuu na Serikali katika Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza jijini Dar es Salaam leo na umelifanya Jiji la Dar kuwa moto kutokana na pilikapilika za ujio wa viongozi mbalimbali.
Licha ya ujio wa viongozi hao wanachama wa SADC, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abbasi alisema tayari mabalozi 42 wa Tanzania wanaowakilisha katika nchi mbalimbali duniani wamewasili nchini kushiriki mkutano huo, hivyo kuzidi kulifanya Jiji la Dar kuzidi kuwa na wageni lukuki.
Pilikapilika za viongozi hao wa SADC zilianza kwa kuwasili Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye alifika nchini Jumatano usiku kwa ziara ya siku mbili ambapo ameunganisha na mkutano huo.
Rais Ramaphosa alipokelewa rasmi na Rais Dk. John Pombe Magufuli juzi Alhamisi katika viwanja vya Ikulu ambapo alikagua gwaride na kupigiwa mizinga 21. Viongozi wengine 14 walitarajiwa kuwasili jana.
Rais Magufuli ambaye anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo, amewakaribisha wafanyabiashara wa nchi hizo wanachama kuja kuwekeza nchini humo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo sekta za afya, hoteli, utalii wa fukwe na uchakataji wa madini.
“Kupitia Rais Ramaphosa, nimewaalika wafanyabiashara kuja kujenga viwanda nchini ikiwemo viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vya madawa na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye madini,” alisema Rais Magufuli.
Wafanyabiashara zaidi ya 1000 wamejitokeza na kuonesha bidhaa zao kwa viongozi hao, hali inayofanya Dar kuwa na mandhari tofauti hasa katikati ya jiji.
SADC hivi sasa inaundwa na nchi wanachama ambazo ni Afrika Kusini Angola, Botswana, Comoro, DR-Congo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Tanzania, Zambia na Zimbabwe. Tanzania iliwahi kuwa mwenyeji wa SADC mwaka 2003 rais akiwa Benjamin William Mkapa.
STORI: Elvan Stambuli, Risasi Jumamosi.
Comments are closed.