The House of Favourite Newspapers

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Apokea Mipira 500 Kutoka TFF Kwaajili ya Kuendeleza Vijana

0
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob Mkunda sehemu mipira hiyo.
Dar es Salaam, 5 Agosti 2024: Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Jacob Mkunda leo amepokea mipira 500 kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Wallace Karia ikiwa ni ahadi aliyoitoa kwa mkuu huyo wa majeshi siku kadhaa zilizopita.
Akizungumza wakati wa kupokea mipira hiyo, Jenerali Mkunda alimshukuru sana rais huyo kwa kutimiza ahadi hiyo ambayo itakwenda kusaidia kukuza vipaji vya vijana kwenye shule za majeshi. Jenerali Mkunda aliendelea kusema;
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob Mkunda akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TFF baada ya kupokea msaada huo.
“Tunaona jinsi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa bega kwa bega kwenye masuala ya michezo, hiyo ni bahati kubwa sana kuwa na kiongozi wa juu kama huyo ambaye anashiriki masuala ya michezo bega kwa bega kwa kiwango cha juu katika kutia hamasa kwenye timu zetu haswa zinaposhiriki michuano ya kimataifa hivyo basi kwa tukio hili ni kumuunga mkono.
“Hivyo basi kwa msaada huu mliotuletea kwetu tumeona hii neema kubwa sana  kwasababu tumetambua kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu limetambua kuwa jeshi ni wadau wakubwa wa michezo.
“Na kwakuwa sasa hivi tuna akademi mpira wa miguu hivyo basi mipira hii itapelekwa huko kwaajili ya kwenda kutumika kufanyia mazoezi.” Alisema Jenerali Mkunda.
Rais wa TFF Wallace Karia (mwenye suti katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda na maofisa wengine wa jeshi wa ngazi za juu.
Kwa upande wake rais Karia amesema kuwa wataendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kuwapa vifaa vitakavyokwenda kutumika kwenye akademi za jeshi hilo zitazoanzishwa hapa nchini ili kuwekeza kwenye mpira wa miguu.
“Hii ni ahadi ambayo TFF tuliitoa na leo tumeitimiza kwa kutoa mipira hii 500.
“Pamoja na yote naomba nitumie nafasi hii kuliomba jeshi nalo kama kunauwezekano mtusaidie kuboresha  baadhi ya viwanja vya soka ikiwemo Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma ambao unatumiwa na timu yenu ya Mashujaa na chenyewe japo kiwekwe taa kama Viwanja vya Kaitaba, Majaliwa, Jamhuri Dodoma na Mkwakwani. “Alimaliza kusema rai Karia.
Leave A Reply