The House of Favourite Newspapers

Mkuu Wa Mkoa Wa Iringa Apokea Msaada Wa Vifaa Vya TEHAMA Kwa Shule 14 Kutoka Vodacom

0
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mh. Halima Dendego (wa pili kulia) akitazama wanafunzi wa shule ya sekondari Mtwivila wakitumia mojawapo ya kompyuta walizosaidiwa na Vodacom Tanzania Foundation ikiwa ni sehemu ya mradi wa uunganishwaji wa shule za sekondari unaolenga kuziunganisha shule 300 Tanzania, (school connectivity project), kwa kushirikiana na African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Taasisi hiyo ilikabidhi kompyuta 31 na vifaa vingine vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89 kwa shule 14 za sekondari mkoani Iringa wiki hii. Pamoja naye wa kwanza kulia ni Mkuu wa Vodacom Nyanda za Juu Kusini, Happiness Shuma, na wa kwanza na wa pili kushoto ni Meneja wa Maduka, Dorice Wambagi, na Msimamizi wa Ripoti, Pendo Mongi, wote kutoka Vodacom.

Iringa – Aprili 25, 2023. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Halima Dendego amepokea msaada wa vifaa 49 vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89 kwa shule 14 kutoka Vodacom Tanzania Foundation ikiwa ni mpango wa uunganishwaji wa shule kwa kushirikiana na shirika la African Child Projects na mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao unalenga kuzifikia shule 300 za umma nchini kote katika awamu hii ya pili.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mtwivila, Mkuu wa Mkoa Iringa, Mheshimiwa Halima Dendego amepongeza juhudi za taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation zinavyoenda sambamba na malengo ya serikali katika kuboresha sekta ya elimu na mafunzo ya kidijtali nchini.

“Bado kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu kwenye sekta ya TEHAMA nchini ambao lazima waandaliwe katika hatua za awali. Mara nyingi wanafunzi huchukia masomo ya michepuo ya sayansi na teknolojia kwasababu ya kukosa maandalizi mapema na vifaa vya kujifunzia. Lakini kwa kuanza kujifunza na kujisomea kupitia vifaa vya TEHAMA wakiwa sekondari itawajengea uwezo na ari ya kuona kuwa kila kitu kinawezekana,” alisema Mh. Dendego

Mkuu wa Mkoa aliongezea kuwa mpango wa uunganishwaji wa shule na mfumo wa TEHAMA unaleta chachu kwenye uboreshaji ufundishaji na kujifunza kwa walimu na wanafunzi. Kupitia TEHAMA ni rahisi kwa walimu kuandaa masomo yao na kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

“Ni matumaini yangu vifaa hivi vya TEHAMA tulivyovipokea kwa hisani ya Vodacom Tanzania Foundation vitaboresha ufundishaji na kujisomea kwenye shule zetu. Walimu bila shaka sasa mtakuwa na uwezo wa kufundisha kwa urahisi na kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya wanafunzi wenu. Wanafunzi nawapa changamoto ya kuondoa hofu kwenye kujifunza, msiviogope vifaa hivi, onyesheni shauku ya kuvifahamu vinatumikaje kwani vitawaandaa kwa masomo yenu kadri mnavyosonga mbele, ”alimalizia Mkuu wa Mkoawa Iringa.

Kompyuta 31, vishkwambi 15, luninga moja, na mashine moja ya kutolea nakala vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 89 vilikabidhiwa kwa shule 14 za sekondari mkoani Iringa ambazo ni Tagamenda, Ipogolo, Miyomboni, Iringa Girls, Lugalo, Mkwawa, Mawelewele, Kihesa, Mazoezi, Mlandege, kwaKilosa, Mivinjeni Idunda, Mlake na Mtwivila. Mpaka sasa wanafunzi takribani 600,000 wananufaika na mpango wa uunganishwaji wa shule nchini kote.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Vodacom Tanzania, Bi. Happiness Shuma alieleza kuwa mradi wa uunganishwaji wa shule nchini ni sehemu ya jitihada za kampuni kutumia mtandao wetu mpana na rasilimali zake katika kusaidia maendeleo ya jamii za Watanzania.

“Msaada wa vifaa hivi vya TEHAMA unaenda sambamba na kuunganishwa kwa intaneti kutoka mtandao wetu SUPA wenye kasi na ufanisi zaidi. Wanafunzi hawa wanayo fursa kubwa ya kuanza kujifunza masomo ya TEHAMA mapema na kukuza ujuzi wao ili kuendana na mapinduzi ya kidijitali.

Pia kupitia mfumo wetu wa e-fahamu wanayo nafasi ya kujisomea na kupata maudhui ya kutosha” alimalizia Bi. Shuma.”

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwivila kwaniaba ya wakuu wa shule zilizonufaika na msaada huo, Dainess Myala alishukuru serikali na Vodacom kwa kusema;

“Ni dhahiri kuwa jitihada hizi za serikali na sekta binafsi zinahitaji kuungwa mkono na shule zote nchini kwa kuhimiza walimu na wanafunzi wetu kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Kama shule, tutakuwa tunatoa mrejesho kwa namna gani vitakavyosaidia katika uboreshaji wa elimu. Ni matarajio yangu kwamba baada ya miaka kadhaa mbeleni shule zote ziwe zinatumia TEHAMA kwenye ufundishaji kwenye ngazi zote kwa kutumia vifaa vinavyotosheleza uhitaji uliopo.”

Programu ya e-Fahamu ilianzishwa na Vodacom Tanzania Foundation mnamo mwaka 2017 kwa lengo la kuwasaidia walimu na wanafunzi wa shule za sekondari kupata vitabu vya ziada na kiada, maudhui ya elimu pamoja na mitaala iliyopitishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania na masomo ya kimataifa bure kwanjia ya mtandao. Lengo la tovuti hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

Leave A Reply