The House of Favourite Newspapers

Mkuu wa Usalama Barabarani Yamkuta, Afutwa Kazi

0
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad Masauni (kushoto) akiwauliza maswali abiria wa basi la Safari Express lifanyalo safari zake Dar es Salaam – Arusha, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Mabasi, Kibaha Maili Moja, Pwani.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amelitaka Jeshi la Polisi kumuondoa katika nafasi ya Mkuu wa Polisi, Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Pwani na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana kwa kushindwa kusimamia sheria za usalama barabarani mkoani humo.

Masauni akiwa ameambatana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Fortunatus Musilimu, alitoa agizo hilo katika Kituo cha Mabasi cha mjini Kibaha Maili Moja baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo leo, kwa ajili ya kufuatilia maelekezo yake aliyoyatoa alipofanya ziara kama hiyo mwaka jana.

Masauni (kushoto) akimuuliza maswali Dereva wa basi la Safari Express.

“Mwaka jana nilipofanya ziara kituoni hapa nilitoa maelekezo nilipokuta kuna mapungufu katika ukaguzi wa magari, tukakubaliana atayafanyia kazi haraka iwezekanavyo, lakini hakuna mabadiliko yoyote, magari hayakaguliwi, huku ni kuhatarisha usalama wa abiria,” alisema Masauni na kuongeza kuwa;
“RTO ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano, nataka aondolewe katika nafasi hiyo na achukuliwe hatua ya kinidhamu, hatutati uzembe, hatutaki kucheza na maisha ya watanzania.”

Masauni (kulia) akimpa maelekezo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi, Jonathan Shana.

 

Masauni mara baada ya ukaguzi wa kituo hicho, aliendelea na ziara yake mkoani Pwani ambapo alifanya ukaguzi wa aina hiyo mjini Chalinze na baadaye Msata na kuimalizia ziara yake Bagamoyo.

Akiwa mjini Chalinze, Masauni alizungumza na waendesha bodaboda na kuwapa maelekezo kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani kwa kutobeba mishikaki, uvaaji wa kofia ngumu na pia kufuata sharia zote za usalama barabarani.

Masauni (kulia) akizungumza na waendesha bodaboda wa Mji wa Chalinze, wakati wa ziara yake.

 

“Mmenihakikishia kwa wale ambao hamkua na kofia ngumu kuwa mkitoka hapa mtakwenda kuzitafuta, hakikisheni mnafanya hivyo kwa usalama wenu pamoja na abiria mnaowabeba, ipendeni kazi yenu kwa kuheshimu sharia za usalama barabarani,” alisema Masauni.

Akiwa njiani kuelekea Chalinze mpaka Bagamoyo, Masauni ambaye gari yake ilitolewa namba zinazomtambulisha nafasi yake (NWMNN), na kuweka namba za kawaida ili kujua kama akiendesha kwa mwendokasi barabarani matrafiki watalisimamisha gari lake, hata hivyo askari wa usalama barabarani sehemu kubwa hawakuwepo barabarani na pia waliokuwepo hawakuweza lisimamisha gari lake.

 

Masauni (aliyevaa suti) akiwa katika ukaguzi wa mabasi katika kituo cha mabasi cha Kibaha Maili Moja, mkoani Pwani ambapo alifanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo.

 

Kutokana na hatua hiyo, Masauni akagundua kuwa kuna uzembe mkubwa unaofanywa na matrafiki mkoani humo kwa kutofanyakazi zao kwa umakini, na kwa uzembe huo ndio chanzo cha ajali zinazotokea barabarani mara kwa mara.

 

Akizungumza na matrafiki wilayani Bagamoyo ambao walifanya uzembe huo, aliwataka wabadilike haraka iwezekanavyo kufuata wajibu wao, na pia alitoa siku tatu kuhakikisha wanawakamata waendesha bodaboda wote ambao wanavunja sheria za usalama barabarani, na pia baada ya operesheni hiyo apewe ripoti haraka iwezekanavyo, na muda wowote atafanya ziara ya kushtukiza kuona kama maelekezo hayo wameyafanyia kazi.

 

Masauni akimpa maelekezo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Fortunatus Musilimu (kulia) wakati alipokua anazungumza na askari wa usalama barabarani katika eneo la Sanzale, Bagamoyo.

 

“Bodaboda nimeziona nyingi zinapita hapa zikiwa zinavunja sheria, madereva na abiria hawajavaa kofia ngumu, na nyie mpo hapa mnaziangalia, sasa nawaagiza mtekeleze maagizo niliyotoa na pia sio nyie tu bali nchi nzima wahakikishe wanayakagua magari pamoja na bodaboda, na atakaepuuza atutacheka nae, tutapambana nae,” alisema Masauni.

Kwa upande wake Kamanda Msilimu, alisema ameyapokea maagizo yote na atahakikisha anayafanyia kazi ipasavyo kwa kuwasimamia matrafiki wote nchini kwa umakini mkubwa.

Leave A Reply