The House of Favourite Newspapers

Mlifeli mipango 2016? fanyeni haya 2017!

couple-wapendanao-mahabaJUMAMOSI ya kwanza ndani ya mwaka 2017. Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuvuka 2016 na kufika salama 2017. Tumuombe baraka zake ili mwaka huu uwe wa mafanikio zaidi!

Kama ilivyo desturi yetu, tunaendelea kupeana elimu ya uhusiano ndani ya ukurasa huu. Kama mada inavyojieleza hapo juu, ulifeli mwaka 2016? Kuna mambo ya kufanya ili mwaka huu uwe wa kihistoria kwako.

Wengi sana hukata tamaa pindi wanapoona mambo hayaendi kama walivyopanga au kukubaliana. Yawezekana mwaka 2016 mlikubaliana kutimiza jambo fulani kama vile kuposana lakini hilo halikutokea. Usikasirike, haisaidii.

Au pengine mlipanga kuona, kwa namna moja au nyingine haikuwezekana, usinune. Ni mipango ya Mungu. Yawezekana mlipanga kwenda kutambulishana kwa wazazi lakini kutokana na sababu fulanifulani, jambo hilo halikufanyika. Usihuzunike.

Pengine mlipanga hivyo kwa takriban miaka miwili, mitatu au zaidi iliyopita lakini katika kipindi chote hicho hamkuweza kutekeleza malengo fulani, msikate tamaa. Mnaweza kutimiza ndoto yenu mwaka huu.

Kutotimiza malengo huwa kunazaa lawama. Utafiti mdogo nilioufanya unaonesha, mara nyingi zaidi wanawake huwaangushia lawama wanaume pindi mipango inaposhindikana.

Wanawalaumu kwa kushindwa kufanikisha jambo ambalo walikuwa wamelipanga, hawataki kupima uzito wa kile kilichowafanya washindwe kutimiza malengo yao. Wanataka kuona matokeo chanya tu!

Wanawake wengi (si wote) hupenda kuona matokeo mazuri, ugumu ambao wanaume wanapitia katika kutimiza jambo fulani wao hawataki kuusikia. Na ndiyo maana wao huwa wanataka kuona ndoto walizojiwekea zinatimia bila visingizio vya aina yoyote.

Hii haimaanishi kwamba wanaume wanaotoa visingizio huwa wako sahihi lakini wakati mwingine huwa wanakuwa na hoja za msingi. Yawezekana mlipata dharura ya jambo fulani kama maafa ya kuunguliwa nyumba, baba au mama mzazi kuugua sana, ajali na mengineyo mazito ambayo kibinadamu yaliwakwamisha.

Ni vyema wapendanao wakasikilizana na kutafuta suluhu ya kweli. Mwandishi mashuhuri, John Mason kwenye kitabu chake cha The Impossible is Possible ameandika: “The person who really wants to do something finds a way; the others find an excuse.” Akiwa anamaanisha, mtu anayetaka kufanya jambo lake, hutafuta njia na si kujitetea.

Ni vyema mkatafuta njia ya kufikia malengo yenu kwa mwaka huu. Suala la msingi ni kuthubutu. Kwa kuwa mlishapanga kufanya, amueni kwa dhati kutekeleza ahadi yenu. Kila mmoja awe na dhamira ya utekelezaji.

Kufikia kile mlichokipanga lazima kuna mahitaji yake. Kuna vitu lazima mvifanye ili muweze kufanikiwa. Itahitajika fedha, lazima mpange mipango mizuri ya kuzipata hizo fedha. Shirikianeni kimawazo, kifikra na hata kifedha pia.

Saidianeni kutafuta njia bora ya kutimiza ndoto zenu. Asiwepo mtu wa kutafuta cha kujitetea. Muwe wawazi katika hili ili kila mmoja aone namna ambavyo mnaweza kufanikiwa au kutofanikiwa. Usiwepo usiri hata kidogo katika njia ya kuelekea kwenye kutimiza ndoto zenu.

Kama wote mnafanya kazi, ni vizuri mkawekana wazi kuhusu kipato chenu. Kama mna biashara ni vyema kila mmoja wenu akatambua kiasi mnachokitengeneza kwa siku, wiki au mwezi. Itasaidia kujua namna sahihi ya kutafuta njia ya kujikwamua.

Mungu ndiYE kila kitu!

Kuna nguvu kubwa sana katika mafanikio endapo tu mtamtanguliza Mungu. Kabla na wakati wa kutekeleza mipango yenu, tekelezeni huku mkiwa mmemuweka yeye mbele. Muombeni awasaidie muweze kuyatekeleza.

Kuweni karibu naye kila hatua, kila wakati. Mnapokuwa naye karibu, anawapa ulinzi. Shetani hawezi kuwajaribu. Hapo mtashuhudia Mungu akiwatendea miujiza yake.

Nikuache na mstari huu wa John Mason; “The devil smiles when we make plans. He laughs when we get too busy. But he trembles when we pray.” (Shetani ana tabasamu tunapopanga mipango. Anacheka mnapokuwa bize kutekeleza mipango lakini anaweweseka pale tunapomuomba.”

Tukutane wiki ijayo hapahapa!

Comments are closed.