The House of Favourite Newspapers

Mlio Wapenzi, Katika Hili Mnajitafutia Mwisho Mbaya!

NI matumaini yangu kwamba umzima na unaendelea vyema na mishemishe zako za kila siku kama kawaida. Kwa wale waislam wenzangu niwape hongera kwa mfungo na kuwakumbusha tu kwamba, wahakikishe swaumu zao zinakuwa timilifu kwa kujiweka mbali na yale ambayo yanaweza kuwaharibia.

Mpenzi msomaji wangu, mapenzi hayana likizo hasa kwa wawili waliotokea kupendana sana. Huwezi kusema unaenda likizo kumpenda mkeo au mpenzi wako lakini kuna wakati unalazimika kuwa mbali naye kutokana na sababu za msingi.

Kama nilivyoanza kueleza hapo mwanzo kwamba, sasa hivi waislam wako katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Wanatubu kwa mola wao kutokana na makosa waliyotenda huko nyuma.

Ni kipindi ambacho hata mke na mume wanazuiwa kukutana kimwili mchana lakini usiku kama kawaida. Kwa wale ambao hawajaoana ndiyo kabisa hawatakiwi kuwa karibu kimapenzi.

Wapo ambao wanamudu kuuheshimu mwezi huu. Hawa ni wale wenye uelewa, wanaojua nguvu ya mwezi huu. Wanajua njia sahihi za kuwasiliana na wapenzi wao na kuhakikisha hawawatibulii swaumu zao. Pia wanawake wanajua wavaeje ili kujisitiri wao lakini pia kutoteteresha swaumu za wanaume wanaopishana nao mtaani.

Wakati hao wakifanya hivyo, wapo ambao naweza kusema ni malimbukeni. Hawa ni wale wasiojua maana ya mwezi huu. Yaani hawana mabadiliko yoyote, kwanza licha ya kwamba ni waislam lakini hawafungi na hata tabia zao hazina tofauti na miezi iliyopita.

Mbaya zaidi ni kwamba, watu hawa wana wapenzi wao ambao wanafunga wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Sasa vuta picha, mwanaume anafunga lakini mpenzi wake hafungi na wala hajui kama mwezi huu unatakiwa uheshimike. Msichana huyo atavaa kihasara na atalazimisha kutaka akutane na mpenzi wake pale anapojisikia.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, msichana huyo akiambiwa na mpenzi wake kuwa amefunga na ni vyema kipindi hiki wakawa mbalimbali, anakasirika na inaweza kuwa tiketi ya kuachana.

Achilia mbali hao, unaweza kukuta mwanaume anajua kabisa mpenzi wake kafunga lakini analazimisha penzi tena mchana kweupe. Kama si kuomba penzi utamkuta mwingine ikifika wikiendi ataomba waende klabu kujirusha na akikataliwa anakasirika.

Jamani, siku 30 siyo nyingi sana, unashindwaje kuvumilia kuwa karibu na mpenzi wako? Iweje ulazimishe mapenzi wakati unajua kabisa kwamba mwenza wako yuko kwenye Mwenzi Mtukufu? Sawa, yawezekana wewe imani yako haukubani lakini mwenzako inambana, kwa nini usimpe ushirikiano afunge bila vikwazo? Na kama wewe ni muislam, hivi kweli hujui dhambi inayoweza kupatikana kama utajiweka karibu na mpenzi wako?

Usitake jamii ukushangae, ni kipindi kifupi tu hivyo usimkasirishe Mungu kwa kufanya makosa ambayo unaweza kuyaepuka.

Hukatazwi kuwasiliana na mpenzi wako na wala siyo vibaya kukutana na kuzungumza mawili matatu yanayogusa maisha yenu. Kinachokatazwa hapa ni kumtega mpenzi wako. Kumvalia nguo ambazo anaweza kukutamani au kumtamkia maneno ambayo yanaweza kumfanya afungue.

Hivi kuna haja gani kumtumia mpenzi wako picha ambazo siyo nzuri kupitia kwenye simu yake? Mchana wa mwezi mtukufu unajipiga picha ukiwa kitandani kimahaba kisha unamtumia mpenzi wako, huku si kumfanyia mwenzako makusudi? Swaumu yake ikikataliwa wewe utafaidika na nini?

Tuache kumchezea Mungu! Kumbuka kwamba kipindi hiki unapomuomba Mungu anakusikiliza zaidi kuliko siku zote. Kitumie kumuomba Mungu aupe uhai uhusiano wenu, kama ni ndoa basi aidumishe, kama ni uchumba, aharakishe ndoa yenu, kama ni wapenzi wa kawaida, awajaalie safari yenu iishie kwenye ndoa.

Niwakumbushe tu kwamba, kama wewe ni muislam na mpenzi wako ni muislam, hakikisha naye anafunga na anatekeleza nguo za swaumu, ukiona anakwenda tofauti na mawazo yako tambua hapo huna mtu, ni vyema ukaachana naye kwani hata mkija kuingia kwenye ndoa mtasumbuana tu.

Kama wewe ni muislam na mpenzi wako ni mkristo, kama kweli anakupenda kwa dhati ataiheshimu swaumu yako na hatakuwa mstari wa mbele kukutibulia. Ukiona anakulazimisha mumuasi Mungu, ujue huyo si mtu mzuri na ana nia ya kukuharibia maisha yako ya sasa na hata maisha baada ya kifo.

Niishie hapo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine. RAMADHAN KAREEM!

Comments are closed.