The House of Favourite Newspapers

MNAOPENDA SANA SUKARI, HII INAWAHUSU!

 WATAALAMU wa afya wanatahadharisha kuwa juhudi zaidi zinahitajika kupunguza kiwango cha ulaji wa sukari kinachotumiwa na watu.  Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ushirikiano na washauri na watafiti wa masuala ya afya nchini Uingereza, wamependekeza kupunguza viwango vinavyopendekezwa vya kutumia sukari mwilini.

Ushauri mpya unasema kuwa kiwango kinachostahili cha sukari mwilini ni asilimia 5 kutoka asilimia 10. Lakini utafiti mbadala unasema kwamba kiwango kinachofaa hakipaswi kuwa zaidi ya asilimia 3 kwa siku. Watafiti wanasema kuwa ushauri huu mpya unahitajika ikizingatiwa gharama ya matibabu kwa sekta ya afya hasa matibabu ya magonjwa ya meno yanayosababishwa na sukari.

Wanasema kuwa sukari ni kiungo muhimu zaidi katika kuchochea magonjwa ya meno kuoza kwa sababu ya hilo, ni ugonjwa ambao unaweza kuzuilika. Kutumia kiwango kikubwa cha sukari mwilini kunaongeza uwezekano wa meno kuoza na kuharibika hususan kwa watoto.

Kwa sasa vipo vyakula vingi sana ambavyo vimekuwa na sukari na tunavitumia karibu kila siku. Kwa bahati mbaya au nzuri vyakula hivi vya sukari vimekuwa vikipendwa na wengi bila kujali madhara yake kiafya yakoje. Kwa sababu hiyo ndani ya makala haya, tutakueleza kinagaubaga sababu ya msingi ni kwa nini unatakiwa uache kutumia sukari kwa wingi mwilini mwako na ikiwezekana kuacha kabisa baadhi ya matumizi ya vitu vyenye sukari nyingi sana.

Matumizi ya sukari kwa wingi ni chanzo kimojawapo cha kuongezeka kwa uzito, lakini si hivyo tu sukari inapokuwa nyingi mwilini inaweza kusababisha kupata magonjwa kama vile ya moyo na kuongezeka kwa shinikizo la damu jambo ambalo ni hatari kwa afya yako kwa kiasi kikubwa. Mara nyingi wanaoutumia sukari kwa wingi sana au wale ambao viwango vya sukari vimeongezeka mwilini mwao, moja ya madhara yake kwa baadaye ni kutokuona vizuri.

Hilo hutokea kwa sababu, sukari inapokuwa nyingi husababisha lensi ya jicho kuongezeka na matokeo yake matatizo ya macho huanza kujitokeza kwa mhusika. Watoto wengi wanaotumia miwani ya kusomea inawezekana ni kutokana na kutumia sukari nyingi. Acha kumpa mtoto juisi za viwandani na pipi kwa wingi.

Tumeeleza hapo juu na mara nyingi hutokea sana kwa watoto, meno huweza kuoza baada ya matumizi ya sukari kwa wingi hasa pipi na ice cream. Kinachotokea ni kuwa sukari huzalisha bakteria wenye sumu ambapo hao huweza kuharibu meno kwa kuozesha. Bakteria hao wanaosababisha kuoza kwa meno ni sehemu ya wadudu wakazi wa kinywani waitwao oral flora. Wadudu hawa hujishikiza kwenye meno na kufanya utando, wana uwezo wa kuchachua vyakula hasa vyenye asili ya sukari na kutoa tindikali.

Ni tindikali hii ambayo huvuta madini kwenye meno na kuweka matobo. Utando huu wa wadudu kwenye jino moja unaweza kuwa na wadudu nusu bilioni, miongoni mwao wakiwemo jamii ya mutans streptococci ambao kimsingi ndiyo wasababishaji wakuu wa kuoza kwa meno. Wale wote ambao sukari inakuwa imeongezeka miili yao inakuwa haina uwezo wa kukabiliana na magonjwa. Sukari nyingi mwilini huwa na tabia ya kuua seli nyeupe ambazo husaidia kupambana na magonjwa. Kwa hali hiyo ndio maana watu wenye visukari hawaponi vidonda kwa sababu kama hii.

Comments are closed.