The House of Favourite Newspapers

MO AANZA STAILI MPYA YA USAJILI SIMBA

Msemaji wa Simba SC Haji Manara (kushoto) akiwa na Mohammed Dewji ‘MO’ .

 

USAJILI mpya wa Simba safari hii utafanyika kwa staili ya aina yake tofauti na misimu mingine iliyopita ambayo Mohammed Dewji ‘MO’ alikuwa pembeni akiwezesha tu.

 

Simba ambao ni mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara wanaojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Desemba mwaka huu, kwa sasa wapo nchini Kenya wakishiriki michuano maalum ya SportPesa.

 

Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba MO ameamua kwamba kila kitu kitakuwa ni siri sana na hakutakuwa na staili ya kamati kama ilivyokuwa misimu iliyopita.

 

Habari zinasema kwamba MO anaifanyia kazi ripoti ya kocha kwa kushirikiana kwa karibu sana na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah na viongozi wengine hawajui kinachoendelea kwenye usajili.

“Sasa hivi hakuna mambo ya watu wengi, MO ameamua kwamba kila kitu atafanya yeye na Salim. Viongozi wengine na wenyewe wanafanya kushtukizwa tu ndio maana huoni mambo mengi yakivuja,”alidokeza mmoja viongozi waliokuwepo kwenye kamati ya usajili ambayo kwa sasa haina meno.

 

Habari zinasema kwamba MO ameamua kufanya hivyo ili kuondokana na tabia za baadhi ya viongozi kusajili wachezaji kwa fedha nyingi na kujipatia cha juu wakati wachezaji wenyewe uwezo wao ni wa kawaida.

 

MO ambaye wanachama wameridhia apewe hisa asilimia 49 ndani ya Simba, amepania kusuka kikosi imara ambacho kitaleta ushindani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

 

Katika utaratibu huo mpya pia wachezaji wapya hawatatambulishwa bila ya kuvalishwa jezi rasmi za mdhamini ambaye ni SportPesa huku ikidaiwa kwamba picha za usajili wa Adam Salamba zilizagaa kimakosa.

 

Staili mpya ya utendaji ya MO inamaanisha kwamba vigogo wa kamati ya usajili sasa wamekaa pembeni akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zacharia Hanspoppe ambae inadaiwa yupo nje ya nchi muda mrefu kwa shughuli binafsi.

 

Habari za uhakika zinasema kwamba MO amewaagiza mawakala wake wamtafutie straika wa maana wa kigeni na yuko tayari kulipa mpaka Shilingi milioni 400 kama ni mtu wa kazi na mwenye umri sahihi.

 

Mpaka sasa Simba imeshamsajili, Salamba kutoka Lipuli, Marcel Kaheza kutoka Majimaji na Mohammed Rashid wa Prisons ambao wote ni mastraika.

 

Kuhusu Kocha Pierre Lechantre, habari zinasema kwamba msimamo wa kumuondoa uko palepale na wamekwenda nae Kenya kwa vile mkataba wake unamalizika mwezi huu.

 

MO tayari ameanza kusaka makocha kutoka katika nchi za Ulaya Kaskazini na Ubelgiji ambapo anataka kocha ambaye ataendana na kasi ya Simba mpya pamoja na kutengeneza mikakati ya kuinua na programu za vijana.

Stori; MARTHA MBOMA

Comments are closed.