Mo Adondosha Milioni 125 Simba

DAR ES SALAAM: JUZI uongozi wa Simba ulifanya hafla ya kutoa tuzo kwa wachezaji wake waliofanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu Bara pamoja na ile ya Kombe la FA msimu uliopita, lengo likiwa ni kuwapongeza wote waliotoa mchango wa aina yoyote kwa ajili ya mafanikio ya klabu hiyo huku Mohammed Dewji ‘Mo’ akielezwa alitoa zaidi ya Sh 125m kwa ajili ya motisha tu.

Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka hapa nchini pamoja na wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya ligi kuu lakini pia ikinyakua ubingwa wa Kombe la FA.

Katika hafla hiyo, Rais wa Simba, Evans Aveva alimtangaza mwanachama na mfadhili wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ kuwa shujaa wa klabu hiyo kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa msimu uliopita kwa wachezaji wa timu hiyo na kuiwezesha kupata mafanikio hayo iliyopata.

Alisema, katika msimu huo, Mo aliwapatia wachezaji kiasi cha Sh milioni 125 kwa ajili ya kuwahamasisha kufanya vizuri uwanjani katika mechi zote za ligi kuu na Kombe la FA walizocheza.

“Mo alifanya kazi kubwa sana, kwa hiyo tunapongeza hilo na tumemzawadia cheti kutokana na kuutambua mchango wake ndani ya Simba.

“Lakini pia tunawapongeza wanachama, wapenzi pamoja na mashabiki wetu ambao pia walijitolea michango yao kwa ajili ya kuwahamasisha wachezaji kupambana vilivyo uwanjani ambapo nao kwa upande wao waliweza kuchangia kiasi cha Sh milioni 125,” alisema Aveva.

Katika hatua nyingine beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alitangazwa kuwa mchezaji bora wa timu hiyo wa msimu uliopita na kuzawadiwa kitita cha Sh 1,000,000 ambazo alizigawa kwa wachezaji wenzake akisema kwa unyenyekevu kuwa hakucheza peke yake uwanjani.

Hivi karibuni pia, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtangaza Tshabalala kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kutunukiwa kitita cha Sh milioni 10.

Ibrahimu Mussa | CHAMPIONI JUMATATU

Spoti Hausi: Mzee Akilimali Atoa ya Moyoni Kuhusu Manji

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment