Mo afanya jambo Simba

BAADA ya Simba kuanza msimu huu kwa matokeo yasiyoridhisha, klabu hiyo imeamua kuunda kamati ya vigogo watatu ambao watakuwa maalum kwa ajili ya kurudisha hamasa kikosini hapo.

 

Vigogo hao ni mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, Salim Abdallah ‘Try Again’ (Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba) na Kassim Dewji ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo.

 

Timu hiyo ikiwa imecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara, tayari imekusanya pointi 11 ambapo imeshinda mechi tatu na kufunga mabao matatu, huku sare zikiwa mbili.

 

Pia imeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

 

Chanzo kutoka Simba, kimeliambia Spoti Xtra, kwamba, mabosi hao wameamua kufanya hivyo muda mchache baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo uliochezwa Novemba 3, mwaka huu ambao Simba walishinda 1-0.

“Kutokana na kutoanza msimu vizuri, hatimaye mabosi wa Simba wameunda kamati maalum ya vigogo tu, itakayokuwa chini ya Mo Dewji, baada ya hivi karibuni kumalizika kwa mchezo dhidi ya Namungo FC.

“Kamati hii ni maalum kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye mchezo wetu dhidi ya Red Arrows na mingine ijayo.

“Vigogo ambao wanaunda kamati hiyo ni Mo Dewji, Kassim Dewji na Try Again,” kilisema chanzo hicho.

Spoti Xtra lilimtafuta Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, ambapo alisema: “Naomba utambue kwamba, siku zote uongozi umekuwa kwenye ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha mambo yote yanayokuwa mbele yetu yapo sawa katika michezo yetu.”

MUSA MATEJA NA LEEN ESSAU, DAR


Toa comment