The House of Favourite Newspapers

Mo Afuata Mastraika Wawili Matata

UONGOZI wa Simba chini ya mwekezaji, Mohamed Dewji ‘Mo’, umepanga kufunga usajili kwa kusajili washambuliaji wawili profesheno kutoka nchi za ukanda wa Afrika.

Wakati usajili ukiwa umefunguliwa Juni 15, Simba imeshafanikiwa saini za washambuliaji wapya, Adam Salamba, Marcel Boniventure na Mohamed Rashid.

Wakati Simba ikipanga kusajili washambuliaji hao, tayari ina Mganda, Emmanuel Okwi na John Bocco wanaoiongoza safu hiyo ya ushambuliaji ambao walikuwa tegemeo katika msimu uliopita.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kutoka kwenye Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Simba inapanga kusajili washambuliaji maalum kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki baadaye mwaka huu.

Mtoa taarifa huyo alisema, washambuliaji hao wanaowataka ni kutoka ukanda wa Afrika Magharibi wenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa Afrika.

Aliongeza kuwa, malengo ya Mo aliyoyaweka ni kuhakikisha timu hiyo inafika katika hatua nzuri ya michuano ya kimataifa Afrika, pia kuuchukua ubingwa wa ligi kwa mara ya pili mfululizo.

 

Pia Simba wamedhamiria kutimiza kauli ya Rais John Pombe Magufuli ambaye katika hafla ya kuwakabidhi kombe la Ligi Kuu Bara, alizitaka timu za Tanzania zilete ubingwa wa Afrika.

“Mo ana mipango mizuri na Simba na kikubwa yeye anaangalia kwenye michuano mikubwa Afrika, kama unavyofahamu timu yetu mwakani inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ni lazima atengeneze kikosi imara kitakacholeta ushindani.

“Hivyo, amepanga kusajili washambuliaji wawili matata kutoka ukanda wa Afrika Magharibi wenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano hiyo mikubwa Afrika.

 

“Ndiyo sababu ya kusajili washambuliaji hao watakaokuwa mbadala wa Okwi na Bocco, kikubwa anataka kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji kama ikitokea akaumia au akapata adhabu ya kadi mshambuliaji mmoja, basi awepo mwingine nje katika benchi atakayeingia na kuziba pengo lake,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Kaimu wa Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliwahi kuliambia Championi kuwa: “Simba tuna uwezo wa kusajili mchezaji yeyote Afrika tutakayemhitaji kwa gharama yoyote.

“Hivyo, kamati yetu ipo kwenye usajili makini katika kukisuka kikosi kitakachokuwa imara kwa ajili ya michuano ya Afrika na ligi.

 

“Tayari tumefanikiwa kuwasajili Salamba, Rashid na Marcel katika safu ya ushambuliaji, hivyo tumepanga kuendelea na usajili kwa kuziboresha baadhi ya sehemu zenye upungufu kwa mujibu wa ripoti ya kocha wetu aliyotupatia ikiwemo safu ya ushambuliaji,” alisema Abdallah.

 Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.