The House of Favourite Newspapers

Mo Akabidhiwa Mzigo wa Mamilioni Simba

0

MWANACHAMA wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, endapo atafanikiwa kuimiliki klabu hiyo, atakutana na mzigo wa kulipia madeni ya kodi klabuni hapo ambayo hadi sasa yanafikia takriban Sh milioni 500. Mo yupo mbioni kuimiliki Simba iwapo pande hizo mbili zitafikia makubaliano ambapo awali bilionea huyo alitaka apewe asilimia 51 za hisa kwa dau la Sh bilioni 20, mchakato ambao unaendelea hadi sasa, ukiihusisha pia serikali.

Mmoja wa vigogo wa Simba ambaye hakupenda kuanikwa jina lake, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, moja ya mipango ambayo imepangwa iwapo Mo atafanikiwa kupewa Simba, atakutana na madeni.

“Tunasubiria ligi iishe, moja ya mipango yetu ni kuona timu inafanikiwa kutwaa ubingwa ambapo baada ya kuupata ndiyo tutaanza mchakato wa kujadili suala la Mohammed Dewji ‘Mo’. “Pesa ambazo zitatumika ni pamoja na bilioni 20 atakazozitoa, lakini kwa sasa mtazamo wote upo kwenye ligi kuhakikisha tunafanikiwa kufanya vyema katika msimu huu unaoenda mwishoni.

“Kwa sasa klabu ipo katika mchakato wa kulipa deni la kiasi cha shilingi milioni 500 za jengo ikiwa ni kodi ambayo haijalipwa kwa muda mrefu huku tulitakiwa kulipa shilingi milioni 45 kwa mwezi TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) lakini tunaendelea vyema katika kulipa.

“Tunatarajia mara baada ya bilionea huyo kukabidhiwa timu kila kitu kitakwenda sawa, kwani mchakato unaonekana kwenda vizuri,” kilisema chanzo hicho. Alipoulizwa Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema: “Kuhusiana na suala la mchakato wa Mo kukabidhiwa timu, uko wizarani na mchakato utakapokamilika, tutarudishiwa ripoti na kuendelea na mchakato.

“Kuhusiana na suala la malimbikizo ya jengo ni kweli yapo na tunaendelea kulipa, lakini kuhusiana na suala la Mo kulipa, tutafanya tathmini ya kila kitu ambacho kipo, kama kuna madeni na mambo mengine atakabidhiwa yeye na kuwa jukumu lake.

Leave A Reply