Mo Ampa Gomes Jukumu la Kushusha Vifaa Vipya

BAADA ya kutolewa katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo’ umempa jukumu zito kocha wao Mfaransa, Didier Gomes la kusimamia usajili wa wachezaji wake wapya.

 

Hiyo ni katika kuhakikisha anakuwa na kikosi bora na imara cha ushindani kitakachompa matokeo mazuri katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kocha huyo tayari ametoa mapendekezo ya usajili ya wachezaji wake wapya katika kukiimarisha kikosi hicho na jumla ya wachezaji wanne kutoka nje ya nchi maalum kwa ajili ya CAF.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kila kitu kinachohusiana na usajili wameliachia Benchi la Ufundi la timu hiyo, linaloongozwa na Kocha Gomes.

 

Try Again alisema kuwa benchi la ufundi ndiyo linalojua upungufu wa timu, hivyo hawatamuingilia kocha katika mapendekezo yake ya usajili katika msimu ujao.

 

Aliongeza kuwa kikubwa wanataka kufikia malengo makubwa katika michuano ya kimataifa msimu ujao baada ya mwaka huu kutimiza malengo ya kufika hatua ya robo fainali.

 

“Katika kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao, uongozi tumedhamiria timu yetu kufika mbali ikiwemo kucheza fainali baada ya mwaka huu kufanikiwa malengo yetu ambayo ni kucheza robo fainali.

 

Hivyo basi tumejifunza mengi mwaka huu baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na kati ya hayo ni kuwa na kikosi bora kitakachotufikisha katika sehemu nzuri.

 

“Ili tuwe na kikosi bora ni lazima tufanye usajili mzuri utakaosimamiwa na benchi la ufundi ambalo lenyewe ndilo limeona upunguzu wa kikosi chake, hivyo kila kitu tutamuachia kocha wetu Gomes katika usajili wa msimu ujao,” alisema Try Again.

STORI: WILBERT MOLANDI, DAR


Toa comment