Mo Amwaga Mamilioni Mwarabu Afe

SIMBA chini ya mwekezaji bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’, imewatangazia wachezaji na benchi la ufundi motisha ya Sh milioni 400 kama wataifunga Al Ahly ya Misri kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar kaitka mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

 

Kunogesha utamu wa mtanange huo, nahodha na mshambuliaji mkongwe wa Simba, John Bocco, amerejea uwanjani na yupo fiti kwa asilimia mia moja kuwavaa Ahly.

 

 

Wakati mshambuliaji huyo akirejea, wachezaji sita wa timu hiyo, Ally Salim, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Ame Ibrahim, Jonas Mkude na Larry Bwalya nao wamejiunga na kambi ya timu hiyo sambamba na kuanza mazoezi ya pamoja wakitokea Kinshasa, Congo ambako walizuiwa kwa kile kilichotajwa kuwa walikuwa na Covid 19.

 

 

Simba kesho inatarajiwa kuikaribisha Al Ahly katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kabla ya mchezo huo, viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba inayoongozwa na Mo, leo Jumatatu inatarajiwa kukutana na wachezaji wa timu kambini kwao Ndege Beach nje kidogo ya jijini Dar es Salaam.

 

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kikao hicho kitakwenda sambamba na kula chakula cha jioni na lengo ni kuwapa morali wachezaji hao katika kuhakikisha wanapata ushindi.

 

 

“Ni mara chache kuwaona viongozi wakifanya kikao na wachezaji tangu kuanza kwa msimu huu, lakini katika kuelekea mchezo huu dhidi ya Al Ahly viongozi wamepanga kukutana na wachezaji kesho (leo) kambini.

 

 

“Lengo ni kuwaongezea hamasa katika kuelekea mchezo huo muhimu kwa Simba kupata matokeo mazuri ya ushindi ili kuhakikisha wanafakikisha malengo yao ya kufika angalau hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa.

 

 

“Katika kikao hicho itatolewa ahadi ya wachezaji kama wakifanikiwa kupata ushindi, kama unakumbuka mchezo dhidi ya AS Vita walipewa Sh 150Mil baada ya ushindi wa ugenini wa bao 1-0 walioupata, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kufikia Sh 400Mil kama wakifanikiwa ushindi na hiyo ni kutokana na ukubwa wa timu inayocheza nayo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

 

Aidha katika hatua nyingine Bocco amerejea kikosini na kuanza mazoezi tangu timu hiyo iliporejea jijini Dar es Salaam ikitokea Congo kucheza na AS Vita.

 

 

“Bocco yupo vizuri na tayari kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Ahly baada ya kupata nafuu ya majeraha yake ya goti ambayo yamemkosesha mchezo uliopita dhidi ya AS Vita.

 

 

“Hivyo atakuwa sehemu ya kikosi hicho kama kocha akimhitaji kumtumia katika mchezo huo wa nyumbani ambao ni muhimu kwa timu kupata ushindi,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

 

Alipotafutwa Meneja Mkuu wa timu hiyo, Abbas Ally kuzungumzia maandalizi ya mchezo huo alisema: “Timu kesho (leo) itafanya mazoezi yake ya mwisho saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

 

“Maandalizi ya mchezo yanakwenda vizuri na vijana wapo katika morali kubwa ya kuhakikisha tunapata matokeo ya nyumbani ambacho ndiyo muhimu,” alisema Ally.

Toa comment