Mo amwaga mamilioni Simba SC

BILIONEA na mwekezaji mkuu wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameendelea kufanya kufuru ya fedha kwenye timu hiyo baada ya kutoa ahadi ya milioni 40. Mo amewaambia Simba kuwa anachotaka ni kuwaona wakitinga kwenye hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya hapo waende wakachukue chao.

 

Hivi karibuni Mo alitoa kitita cha maana kwa wachezaji wa timu hiyo baada ya kuitandika Mbabane Swallows katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo inaelezwa kuwa alitoa Sh milioni 30 kwa wachezaji hao.

 

Hata hivyo, habari za kuaminika ambazo Championi Jumatano limezipata kutoka ndani ya Simba, zimedai kuwa kuanzia sasa wachezaji wa timu hiyo watakuwa wakilamba milioni 40 kila watakapofanikiwa kutoka hatua moja na kwenda hatua nyingine ya michuano hiyo.

 

Jana Simba walikuwa wanacheza mechi ya pili dhidi ya Mbambane Swallows ambapo kama wangeshinda wana uhakika wa kulamba mamilioni hayo ya fedha.

 

“Ahadi hiyo alitupatia hivi karibuni kabla ya kuja Swaziland kupambana na Mbabane Swallows na atakuwa akifanya hivyo endapo tu tutakuwa tukifanikiwa kutoka hatua moja ya michuano hii na kwenda hatua nyingine.

 

“Kwa hiyo, kazi ni kwetu sasa kuhakikisha tunapambana vilivyo ili kufanya vizuri katika kila mechi,” kilisema chanzo hicho cha habari. Hata hivyo, mbali na fedha hizo ambazo watakuwa wakizipata katika michuano hiyo ya kimataifa, lakini pia katika michuano ya Ligi Kuu Bara wachezaji wao wataendelea kulamba Sh milioni 30 kila watakapokuwa wakishinda mechi tatu mfululizo kutoka wa bilionea huyo.

 

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema kuwa: “Ni kweli kuna fedha ambayo watakuwa wakipata kila baada ya hatua moja lakini siwezi kusema ni kiasi gani, hiyo ni kwa ajili ya kuwahamasisha kuhakikisha tunafanya vizuri katika michuano hii ambayo ni mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.”

Toa comment