Mo Amwaga Mil 85, Gari kwa Mwamnyeto

HATIMAYE imefichuka rasmi kuwa uongozi wa Simba chini ya tajiri Mohammed Dewji ‘Mo’ umemuwekea mezani ofa ya shilingi milioni 85 na gari aina ya Toyota Crown, beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Nondo Mwamnyeto ili tu ajiunge na kikosi hicho.

 

Beki huyo wa kati wa Coastal Union ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho, msimu huu amekuwa kwenye kiwango kizuri kiasi cha kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ chini ya kocha Etienne Ndayiragije.

 

Ikumbukwe hivi karibuni Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alilalamikia safu yake ya ulinzi yenye wachezaji wakongwe kama Erasto Nyoni, Pascal Wawa, kuruhusu mabao mengi.

 

Taarifa ambazo limezipata Championi Jumamosi kutoka ndani ya Simba ni kuwa, mabosi wa timu hiyo kwa sasa macho yote wameelekeza kwa Mwamnyeto katika kuhakikisha wanamalizana naye kabla ya wapinzani wao kuwawahi.

 

Chanzo kiliendelea kutiririka kuwa, kasi ya usajili wa mchezaji huyo inatokana na ombi la kocha Sven kwa uongozi kuwa uongeze beki wa kati mwenye umri mdogo ambaye ataweza kuisaidia timu hiyo katika eneo la ulinzi.

 

Hivyo baada ya hapo chaguo la kwanza likawa kwa Mwamnyeto ambaye ana umri mdogo, pia anaonekana kuanza kuiva kwa maana ya kupambana mbele ya mastraika wakali na wenye miili mikubwa.

 

“Katika eneo la ulinzi la Simba, kocha alipendekeza kuwa atafutwe beki mwingine mwenye umri mdogo ambaye pia ana uzoefu kidogo na michezo ya nje ya nchi ambaye ataweza pia kutumika katika michezo ya kimataifa ili aje kuongeza nguvu katika eneo hilo kwa msimu ujao.

“Hivyo uongozi wa Simba umeona kuwa Mwamnyeto ana vigezo vyote vya kocha Sven alivyoviainisha kwa kuwa kwanza ni mdogo kiumri, lakini ana uzoefu tayari katika michezo ya kimataifa kwani akiwa na timu ya taifa tuliona jinsi alivyofanya vyema.

“Tayari beki huyo kashaandaliwa dau nono litakalokuwa si chini ya milioni 85 na nyongeza ya gari aina ya Toyota Crown ambalo tunaamini dili hilo litamleta beki huyo klabuni kwetu,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Dk Arnold Kashembe ambaye ni katibu wa Simba alisema: “Ishu ya usajili kwa sasa bado, siwezi kuzungumza chochote kwani dirisha halijafunguliwa.”

Simba hivi karibuni wamekuwa wakitumia ndoano ya fedha na gari katika kuwanasa wachezaji wanaowataka na walifanya hivyo kwa mastaa kama Adam Salamba kutoka Lipuli FC na Gadiel Michael kutoka Yanga, hivyo wanaamini pia Mwamnyeto hawezi kuchomoa pindi atakapopewa mkoko wake.

Toa comment