The House of Favourite Newspapers

Mo Anunua Bao Sh 200 Mil

0

KATIKA kuwaongezea morali na hali ya kujituma katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, juzi Jumanne alikutana na wachezaji wa timu hiyo na kuahidi kutoa Sh 200 Mil kwa Simba wanaoongoza Kundi A katika michuano hiyo, wakiwa na pointi sita, Jumamosi hii itakuwa ugenini nchini Sudan kupambana na wenyeji wao, Al Merrikh.

 

Timu hiyo jana jioni ilianza safari ya kuelekea Sudan kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na Al Merrikh kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya Al Ahly na AS Vita.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, bilionea huyo aliwapa maneno mazuri ya kuwaongezea morali wachezaji na kikubwa akihitaji ushindi ili kuendelea kukaa kileleni katika msimamo wa kundi lao.

 

Mtoa taarifa huyo alisema wachezaji kwa pamoja walimuahidi bosi huyo kwenda kupambana na kurejea nyumbani na pointi tatu ili kufanikisha malengo ya kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.Aliongeza kuwa, mamilioni hayo wameahidiwa kupewa mara baada ya timu hiyo itakaporejea nchini ikitokea Sudan.

 

“Wachezaji washindwe wenyewe katika msimu huu, kwani kama wakijitahidi kupambana katika michuano hii mikubwa ya kimataifa, basi watajipatia fedha nyingi kwani kila mechi wanaahidiwa fedha.

 

“Mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly waliwekewa Sh 400Mil kama watawafunga, wakapambana wakapata ushindi na pesa hiyo imekuwa nyingi kutokana na ukubwa wa timu ambayo tuliyocheza nayo.

 

“Na katika kueleke mchezo dhidi ya Merrikh, Mo ameahidi kuwapa wachezaji kitita cha Sh 200Mil kama watafanikiwa kupata ushindi wa ugenini, hii ni baada ya jana (juzi) kukutana na wachezaji na kufanya kikao nao,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Akizungumzia hilo, katibu mkuu wa timu hiyo, Arnold Kashembe, alisema kuwa: “Kila mechi kuna ahadi ya fedha ambayo tunaitenga, hivyo ni kawaida yetu.”

Leave A Reply