Mo Dewji: Jamani… Mkude haendi Yanga

Mohammed Dewji ‘Mo’

SIKU chache baada ya Gazeti la Championi kuripoti kuwa kiungo wa Simba, Jonas Mkude anatakiwa na Yanga, fasta bilionea wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ amemuita na kukaa naye kikao kwa saa 2.

 

Mo baada ya kusikia Yanga imemtengea Mkude kitita cha Sh mil 120, ili iweze kumsajili na kwamba Mei 28, mwaka huu ingemtangaza kama mchezaji wake mpya, hatimaye sasa ameamua kuonyesha jeuri ya fedha kwa kumalizana naye.

 

Alichofanya Mo ni kunyanyua simu yake ya mkononi na kumpigia Mkude kisha kumwambia waonane ofi sini kwake kwa ajili ya mazungumzo ya haraka juu ya mkataba wake mpya.

 

Katika mazungumzo hayo ambayo yanadaiwa kuchukua muda wa saa mbili, Mo alitaka kujua ofa ambayo Mkude amewekewa mezani na Yanga ili aweze kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo.

 

Habari ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa, baada ya maongezi hayo Mo amemuahidi Mkude kumfanyia yote ambayo Yanga wanatarajia kumfanyia atakapojiunga nao. Hata hivyo inadaiwa kuwa Yanga wamepanga kumpatia Mkude mkataba wa miaka miwili ambao thamani yake itakuwa ni zaidi ya Sh mil 312.

 

Imeelezwa kuwa, Simba wamepanga kumpatia mara tu atakaposaini mkataba huo ambayo ni Sh mil 120, lakini baaada ya kusaini hiyo miaka miwili thamani ya mishahara ndani ya muda huo inakadiriwa kufi kia kiasi cha Sh mil 192.

 

Hiyo inamaanisha kuwa kila mwezi atakuwa akikunja Sh mil 8 ambazo ukizizidisha mara miezi 24 ambayo ni miaka miwili utapata Sh mil 192 ambazo ukizijumlisha na zile fedha za usajili Sh mil 120 jumla dau lake litakuwa Sh mil 312. “Mkude amekutana na bosi leo (jana) hiyo ni baada ya kusikia kuwa Yanga wamemtengea donge nono na yeye bila kusita akaamua kumuita ofi sini kwake kwa ajili ya mazungumzo.

 

“Kwa hiyo alichofanya Mo ni kumwambia Mkude atulie kwani kila kitu ambacho Yanga wameahidi kumpatia atakipata akiwa Simba, ila bado hajasaini mkataba,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipotafutwa Mkude ili aweze kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita tu bila ya kupokelewa lakini baadaye alipokea na kusema: “Nitakupigia nipo na bosi,” kisha akakata simu, lakini alipotafutwa baadaye simu yake iliita tu bila ya kupokelewa.

 

Hata hivyo, alipoulizwa Mwanasheria wa Mkude kuhusiana na hilo alisema; “Mkude bado hajasaini mkataba rasmi lakini aliitwa na bosi wake kwa ajili ya mazungumzo baada ya kusikia kuwa Yanga wanamtaka.” Kupitia Mtandao wa Kijamii wa Instagram, Mo Dewji jana aliweka ujumbe unaosomeka kuwa: “Wanasimba msiwe na wasiwasi, Mkude haendi popote.”


Loading...

Toa comment