The House of Favourite Newspapers

 Mobeto, Kiba Wanaswa Hotelini

0

MWANAMAMA anayebeba ‘taito’ tatu kwa mpigo ya uigizaji, mwanamuziki na mwanamitindo maarufu Bongo, Hamisa Mobeto na mwanamuziki Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ wamezua gumzo kama lote baada ya kunaswa kwenye hoteli moja ya kifahari visiwani Zanzibar, mapema wiki iliyopita.

 

Gumzo hilo lilizuka kwenye hoteli hiyo ya kifahari iliyopo eneo la Bubu visiwani humo baada ya wawili hao kutinga hotelini hapo wakiwa na wapambe kibao na ulinzi wa kutosha.

 

WAIBUA MASWALI

Kwa mujibu wa mashuhuda wetu, ishu hiyo iligeuka gumzo na kuibua maswali, kwani inafahamika kwamba, Mobeto ni mzazi mwenza wa hasimu mkubwa wa Kiba, mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’.

 

Baada ya kutonywa ishu hiyo, gazeti hili lilifika kwenye hoteli hiyo na kukuta gumzo hilo ambapo wageni mbalimbali na wahudumu  wa hoteli hiyo, walikuwa wakijiuliza maswali mengi.

 

MOBETO NI MZAZI MWENZA WA MONDI

Walisema kuwa, wanachojua ni kwamba Mobeto yupo karibu na Mondi ambaye siku chache zilizopita walikuwa wanasifiana kwa kuwa wana mtoto wa kiume waliyezaa pamoja aitwaye Dyllan.

 

“Kabla hujafika hapa, tumejiuliza maswali mengi sana, imekuwaje hawa wapo pamoja hotelini, wanakaa, wanapiga stori na wamekuja na wapambe wao wakati tunajua

Mobeto yupo kwa Mondi na ni juzijuzi tu Mondi alimposti Mobeto na kummwagia sifa kama zote?” Alihoji mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.

 

Lakini kwa mujibu wa mmoja wa watu waliokuwa kwenye msafara wa pamoja na wawili hao, Mobeto na Kiba wana ‘project’ mpya kwani wanatarajia kutoa wimbo wa pamoja na wameamua kuja visiwani huku kwa ajili ya kufanya kitu cha tofauti ambacho kitawashtua watu wengi.

 

KUMALIZA UKIMYA

Mmoja wa watu wa Mobeto anayefahamiana na mwandishi wetu aliyekuwa kwenye msafara huo, alitonya kuwa, huo ni ujio mpya wa Mobeto ambapo wimbo huo utatoka mwezi ujao (Aprili) na ndiyo utakaokuja kumaliza maneno mengi juu ya ukimya wa Mobeto na Kiba.

 

Mwandishi wa habari hii, alijaribu kuongea na Mobeto, lakini hakutaka kufanya mahojiano ya muda mrefu na gazeti hili.

“Nimekuja kwa ‘project’ visiwani huku, suala la picha nitaposti kwenye ukurasa wangu usijali,” alisema Mobeto aliyekuwa amevalia maski na gloves kwa ajili ya tahadhari ya kusambaa kwa Virusi vya Mafua ya Corona.

 

MARA YA MWISHO

Mara ya mwisho kwa Mobeto alitoa wimbo mpya ilikuwa ni mwezi Desemba, mwaka jana ambapo aliachia Wimbo wa Nipotezee huku Kiba kwa mara ya mwisho akisikika na kuonekana kwenye Wimbo wa Chaku akiwa na Christian Bella.

 

TUJIKUMBUSHE

Miezi kadhaa iliyopita, Mobeto  alidaiwa kunaswa hotelini maeneo ya Masaki jijini Dar, akiwa na hasimu mwingine wa Mondi, mwanamuziki Rajab Abdul ‘Harmonize’, jambo lililoibua maswali kama alivyonaswa na Kiba.

Hata hivyo, viongozi wa pande zote mbili walikanusha wawili hao kuwa na uhusiano wa kimapenzi zaidi ya ule wa kikazi.

 

MOBETO HAHITAJI USUMBUFU

Kuhusu suala la uhusiano wa kimapenzi, hivi karibuni alilielezea gazeti hili kuwa, hana mwanaume na hahitaji usumbufu.

Alisema kuwa, amekuwa akishangazwa na watu wanaomhusisha na kurudiana na Mondi kitu ambacho si cha kweli, isipokuwa wao ni wazazi hawawezi kuacha kuwasiliana.

 

“Hivi, kumbe watu wanapenda watu waishi kwenye ugomvi miaka yote kitu ambacho siyo sahihi?

“Ningeomba tu, watu wajue mimi sijarudiana na mtu wala sina mpango huo. Kuongea na Esma (dada wa Mondi) siyo tatizo maana ni shangazi kabisa wa mtoto wangu na kama tofauti zetu, tuliziweka pembeni,” alisema Mobeto.

 

Leave A Reply