Mocco Genius Maana Halisi Ya ‘From Zero To Hero’ na Ndoto za kutoboa Kimataifa
KAMA wewe ni kijana mtafutaji basi lazima utakuwa unaufahamu vizuri ule msemo wa ‘FROM ZERO TO HERO’ wenye maana ya kutoka sifuri mpaka kuwa shujaa! Sasa kama kila msemo una mhenga wake, msemo huo ni mali ya mhenga huyu, Iddy Mohamed maarufu kwa jina la Mocco Genius.
Najua Jina la Mocco Genius sio geni kabisa masikioni mwako kwa sababu huyu ni mtayarishaji hodari wa muziki nchini Tanzania, ambaye ametengeneza nyimbo nyingi zinazovuma ndani na nje ya nchi, lakini usichokifahamu ni ule msoto aliopitia prodyuza huyu hadi kufikia hatua ya kuaminiwa na wanamuziki wakubwa akiwemo Diamond, Alikiba na Harmonize.
Mocco Genius ni mtoto wa 4 katika familia yenye watoto 10, alizaliwa katika Wilaya ya Kilwa huko mkoani Lindi, kabla ya wazazi wake kuhamia wilayani Bagamoyo na kuweka makazi yao huko, ambapo ndipo prodyuza huyu alipopata elimu yake ya msingi na sekondari.
Baada ya hapo, hakufanikiwa kuendelea na elimu ya juu, badala yake akaingia kupata elimu mtaani ya kutayarisha muziki ambayo ndiyo iliyomtambulisha duniani.
Haikuwa hahisi kwa Mocco kufaulu mitihani ya elimu mtaani, lakini kumtanguliza Mungu, juhudi na nidhamu ndiyo silaha zilizomfungulia milango ya uaminifu na mwaka 2017 akatengeneza rasmi ngoma za wanamuziki wakubwa akiwemo Chege, Alikiba, Mbosso, Zuchu na Diamond Platinumz.
“Safari ya mafanikio siyo rahisi, nimepitia kukataliwa, kuvunjwa moyo, kukatishwa tamaa, na mambo mengi tu, lakini leo mimi ni prodyuza mkubwa Afrika, na matarajio yangu ni kutoboa anga kimataifa. Kama wasanii wetu wanavyoenda Ulaya kuwafuata maprodyuza wakubwa, basi wasanii wao nao waanze pia kuja Tanzania kutufuata sisi,” amesema Mocco Genius.
Mbali na kutayarisha muziki, Mocco Genius anapenda kucheza mpira na kwa upande wa familia bado ni bachela, hana mke wala mtoto.
Ni matumaini yangu kuwa kupitia makala haya umeweza kumfahamu vizuri Prodyuza Mocco Genius.