The House of Favourite Newspapers

MOI Kulipa Fidia ya Tsh. Mil. 100 kwa Kupasua Kichwa Badala ya Mguu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), kumlipa fidia ya Tsh milioni 100 ndugu Emmanuel Didas kwa kosa la kumfanyia upasuaji wa kichwa badala ya mguu kutokana na madhara aliyoyapa kimwili na fahamu.

 

Mahakama imetoa amri hiyo baada ya Didas kushinda kesi yake ya madai aliyoifungua dhidi ya MOI, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (wakati huo) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo amedai Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa wakati kiungo alichotakiwa kufanyiwa upasuaji huo ni mguu.

 

Jaji Zainabu Muruke alisema Sh. 1,076,620 ni fidia maalumu kwa kukosa kipato kwa kipindi cha miezi 21, tangu Novemba Mosi, 2007 ambapo Didas alifanyiwa upasuaji hadi Agosti 24, 2009 alipoajiriwa na Moi kama mhudumu wa karakana. Didas ambaye ni fundi pikipiki kulingana na ushahidi wake, kabla ya kupewa ajira na MOI alikuwa akijipatia kati ya Sh 15,000 na Sh 25,000 kwa siku moja.

 

Fidia aliyostahili ni baada ya kukokotoa kwa kutumia waraka wa Serikali namba 2 wa mwaka 2007 kuhusu kima cha chini cha mshahara ambapo Sh 10.6 milioni ni gharama za huduma za nyumbani, Sh 88,323,380 ni fidia ya maumivu na mateso aliyoyapata kutokana na upasuaji usio sahihi uliosababishwa na uzembe wa wataalamu katika kumhudumia.

 

 

Pia, alisema iwapo Moi itakatisha mkataba wake wa ajira kwa sababu zozote, italazimika kumlipa mshahara na mafao mengine kwa muda wote atakaokuwa amebakiza kustaafu kwa lazima. Kesi hiyo namba 129 ya mwaka 2012, ilifunguliwa na Sisti Marishay kwa niaba ya Didas kutokana na kupooza.

 

Didas alifanyiwa upasuaji huo usiyo sahihi Moi kutokana na ajali aliyoipata na kuumia mguu, wakati akifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu, mgonjwa mwenzake, Emmanuel Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu ambao haukuwa na tatizo badala ya kichwa.

 

Aidha, Kutokana na makosa hayo, wagonjwa wote wawili walipelekwa katika hospitali ya Indraprastha Apollo, nchini India kwa matibabu zaidi ambapo Mgaya aliaga dunia baadaye.

Comments are closed.