The House of Favourite Newspapers

Molinga Awapa Simba Raha Dar

SIMBA jana walilala na furaha pengine kuliko watu wote Duniani. Kipigo cha Yanga mbele ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Uhuru kiliwafurahisha kwelikweli haswa kutokana na muziki ulioanzishwa na watani wao. Lakini siyo hivyo tu, Simba walionekana kulipiza kejeli za Yanga walizowafanyia baada ya kipigo dhidi ya UD Songo wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam.

 

Katika mchezo wa jana Yanga ilianzisha mastraika wanne kwa mpigo lakini hesabu zikafeli na kushindwa kuchomoa bao 1-0 la Ruvu Shooting ya Masau Bwire. Muziki huo wa Yanga ambao ulimhusisha straika Mkongomani, David Molinga ‘Falcao’ aliyesajiliwa dakika za mwisho, ulikosa nafasi nyingi za wazi na kumpandisha hasira Kocha, Mwinyi Zahera ambaye alifoka sana vyumbani baada ya mechi.

 

Sadat Mohamed ndiye aliyetupia bao la ushindi dakika ya 20 ya mchezo akitumia makosa ya mabeki wa Yanga na kuibua shangwe za aina yake kwa Simba ambao walikuwa wakisubiri kuona maajabu ya mastraika wanne ambao watani wao walikuwa wakiwatambia wakiongozwa na Juma Balinya, David Molinga, Sadney Urikhob na Patrick Sibomana.

 

Licha ya kuonyesha ufundi lakini haukusaidia kubadili matokeo. Maafande hao waliwang’ang’ania Yanga na kuharibu rekodi ya Jangwani ya msimu uliopita baada ya kushinda mechi zake 19 za awali bila ya kupoteza hata moja.

 

Kwenye mechi hiyo Ruvu ambao wanafundishwa na aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga walipata bao la ushindi kupitia kwa Sadat kufuatia makosa ya Kelvin Yondani kuchanganyana na kipa wake Farouk Shikalo ambaye ni raia wa Kenya.

 

Kipa wa Ruvu, Bidii Hussein alikuwa nguzo ngumu kwa kikosi hicho kwa kuondoa mashambulizi kibao ambayo yalipelekwa langoni mwake na kuongeza mbwembwe ambazo ziliongeza burudani kwa mashabiki wa Simba ambao walipata sehemu ya kulipia kisasi kutokana.

Comments are closed.