Molinga, Sibomana, Yikpe nje Yanga
INAELEZWA kuwa uongozi wa Yanga upo kwenye mipango ya kuachana na washambuliaji watatu wa klabu hiyo ambao ni David Molinga ‘Falcao’, Patrick Sibomana na Muivory Coast, Yikpe Gnamien.
Licha ya mchango wa mabao 14 waliyofunga nyota hao katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini uwezo wao umeonekana kutowaridhisha viongozi wa Yanga ambao sasa wamepanga kuachana nao na kufanya usajili wa nguvu utakaoimarisha zaidi safu hiyo ya ushambuliaji.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mtoa taarifa ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa wachezaji hao wameshindwa kuushawishi uongozi ili kuendelea nao.
“Washambuliaji David Molinga, Patrick Sibomana na Yikpe Gnamien wameonekana kutowaridhisha viongozi kwa huduma wanayoitoa licha ya kulipwa pesa nyingi hivyo uongozi kwa sasa umeona ni bora ukaachana nao mwishoni mwa msimu huu.
“Hili litafanyika ili kutoa nafasi ya kusajili wachezaji wengine ambao watakuwa na msaada mkubwa kwenye timu kipindi hiki ikijitahidi kurudisha makali yake ya zamani,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, alisema: “Kwa kweli mimi siyo mwanasheria, hivyo sijui mikataba yao inaelekeza vipi, hiyo inanifanya nishindwe kuliongelea suala hilo, lakini nachokijua mimi ni kuwa klabu yetu ipo katika mchakato wa kujiimarisha zaidi na kuwa na timu imara.”
Joel Thomas, Dar es Salaam


