MONDI AMUUMBUA ZARI UGANDA!

MAMBO ni moto! Bado ‘muvi’ la zilipendwa Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ linazidi kutikisa na safari hii, jamaa huyo amemuumbua mama watoto wake huko nchini Uganda, Gazeti la Ijumaa Wikienda limedokezwa.  Iko hivi, Diamond au Mondi na Zari wiki iliyopita walitinga jijini Kampala, Uganda kwa shughuli za kikazi ambapo matarajio ya mashabiki wa nje ya Uganda na kwingineko yalikuwa ni kuona Mondi anakwenda kula ‘mashuti’ nchini humo, lakini mambo yakawa tofauti.

MVUTANO ULIOKUWEPO

Baada ya tu ya Mondi na Zari kutangaza kuwa watakuwa Uganda kupitia ‘platfom’ zao za mitandao ya kijamii, mashabiki wengi kwenye Mtandao wa Instagram walishambuliana kwa maneno. Kuna ambao walisema Diamond anakwenda kuumbuka nchini humo kwa kuwa hayupo kwenye maelewano mazuri na Zari ambaye huko ni nyumbani kwao, lakini wengine walisema wa kuumbuka ni Zari.

Waliokuwa wanasema Mondi anakwenda kuumbuka, walikuwa wengi zaidi ambapo walikuwa na hoja kwamba wamekuwa wakimuona mkali huyo wa Bongo Fleva si mtu mzuri kwani amekuwa akicheza na wanawake kisha kuwaacha solemba.

WACHACHE WAMTETEA

Pia walikuwepo wachache ambao walimbeba Mondi ambapo walikuwa na hoja kwamba, Waganda wanamkubali Mondi kuliko mtu mwingine bila kujali kwamba amemwagana na ‘dada’ yao (Zari). “Wee yaani Waganda huwaambii kitu kwa Diamond…si unajua tena ushemeji haufi? Wewe utaona jinsi watakavyompokea Mondi kwa mbwembwe kuliko hata Zari,” hayo yalikuwa ni baadhi ya maoni.

ZARI FULL KUMRUSHA ROHO MONDI

Vyanzo vilivyo karibu na Zari vilieleza mitandaoni kuwa, Zari amepania kwenda kumuonesha Diamond kuwa kule ndiyo kwao na shoo yake itakuwa na msisimko na kamwe hakuna mtu atakayefuatilia shoo ya Mondi hivyo itakuwa kama vile hakwenda.

“Zari kaahidi kumuonesha Simba (Mondi) kwamba yeye ana nguvu kiasi gani tena na hivyo ni kwao, ameshaseti watu wake kule wampokee kwa kishindo, aende hotelini kwa msafara mkubwa ili tu kuhakikisha hata vyombo vya habari haviripoti ujio wa Mondi na badala yake vichafue picha zake kila kona na awe gumzo,” vilieleza vyanzo hivyo.

MONDI APINDUA MEZA KIBABE

Tofauti na maoni ya wengi kwenye mitandao hiyo ya kijamii, Mondi alifika nchini humo na kupokelewa kwa bashasha za kutosha kuanzia Uwanja wa Ndege wa Entebbe hadi ukumbini.

Mitandao mbalimbali ya Uganda iliandika kuwa, tofauti na matarajio ya wengi, Diamond alimgaragaza Zari kwa kupata mapokezi mazuri tena ya muda mfupi na kama hiyo haitoshi, kwenye shoo yake alijaza watu wakawa wanamuunga mkono kwa kumshangilia mwanzo hadi mwisho wa shoo.

Ilielezwa kuwa, mashabiki waliofurika kwenye shoo ya Comedy Store iliyofanyika Lugogo nchini humo wengi wao walikuwa hawajui Kiswahili vizuri, lakini waliimba mwanzo hadi mwisho nyimbo kali za Mondi zikiwemo Kanyaga, Inama, Tetema na Kainama. Mashabiki wengi walisikika wakisema wanamtambua Mondi kama shemeji sahihi tofauti na wengine ambao Zari amekuwa akijinasibu nao akiwemo King Bae ambaye anatrendi kwa sasa.

ZARI KAWAIDA SANA

Kwa upande wake Zari, alifika nchini humo na kupokelewa kawaida tofauti na matarajio makubwa aliyokuwa nayo pamoja na wapambe wake. Alipofika Uwanja wa Ndege wa Entebbe, alikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Sheraton ambapo alipewa maua na wamiliki wa hoteli hiyo kisha kujiandaa na kwenye shoo ya Miss Uganda 2019 ambayo ndiyo ilimpeleka.

Mrembo huyo aliyezaa watoto wawili na Mondi alihudhuria shoo hiyo ambapo alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuitwa ‘mama’ na MC wa shughuli hiyo, jambo ambalo lilimfanya kukinukisha usiku huo akiporomo sha maneno makali kwa mshereheshaji huyo.

Mitandao ya nchini humo imeeleza kuwa, Waganda wengi hawakuwa na furaha sana na Zari kwa sababu wanahisi anawapeleka sana chaka katika mambo yake ikiwemo suala la kusema ameolewa wakati hajawahi kumpeleka huyo mwanaume aliyemuoa. Hata hivyo, Zari alijitetea kwa kusema kwamba safari hiyo haikuwa kwa ajili ya kumtambulisha mumewe huyo, bali ilikuwa ni ya kikazi hivyo atampeleka kumtambulisha siku muafaka


Loading...

Toa comment